Uingereza imeandika barua kwa
ubalozi wa Ecuador mjini London ikitaka kurejelea mazungumzo kuhusu
hatma ya Julian Assange, mwanzilishi wa mtandao wa kufichua siri wa
Wikileaks, aliyetorokea katika majengo ya ubalozi huo kuepuka kurejeshwa
nchini Sweden kwa lazima.
Uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ulivurugika
baada ya uamuzi wa Ecuador kumpa bwana Assange hifadhi ya kisiasa na
Uingereza kutishia kuvamia ubalozi huo na kumkamata.
Afisi
inayoshughulika na masuala ya kigeni haijasema chochote kuhusu ujumbe
uliokop kwenye barua hiyo lakini afisa mmoja ameelezea kuwa inanuia
kutuliza hali kati ya mataifa hayo mawili.
Rais Rafael Correa ameiambia BBC kuwa Uingereza
ilifanya makosa makubwa kwa kutishia kuingia kwa nguvu kwenye ubalozi wa
Equador,''Huu ni mvutano ambao ungeisha iwapo Uingereza ingetoa
hakikisho ya kupita kwa usalama kwa Bwana Assange au unaweza kuendelea
kwa miezi na hata miaka iwapo hataweza kutoka kwenye ubalozi wetu hapa
London kuelekea Equador.''
Huenda mataifa ya Amerika Kusini yakamuunga mkono rais Rafael Correa.
Huku Uingereza ikisema kuwa inataka kurejelea
mashauriano kuhusu hatma ya Julian Assange, Equador haikubaliani na
msimamo huo na inataka kuhakikishiwa kuwa Assange hatakamatwa iwapo
atatolewa kwenye ubalozi wao nchini Uingereza kuelekea Equador.
Equador inataka pia kuhakikishiwa kuwa
mwanzilishi huyo wa mtandao wa Wiki Leaks hatawahi kupelekwa Marekani
anakokabiliwa na tuhuma za kutoa taarifa muhimu na za siri kwenye
mtandao wake.
Hata hivyo hakuna matumaini kwamba Marekani itakubali hilo.
Kwa hiyo ubalozi wa Equador umekiri kuwa huenda ukampa bwana Assange hifadhi kwa miaka mingi.
0 comments:
Post a Comment