Ndugu Waandishi,
Nalazimika kukutana nanyi kutoa maelezo juu ya tuhuma zenye shinikizo la kisiasa zinazoelekezwa kwangu binafsi kwamba hata mimi nimeshiriki katika vitendo vya rushwa, kwa nafasi yangu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma. Taarifa hizo, kama kawaida ya uzushi mwingine wowote zimesambazwa kimkakati na kwa kasi kubwa kiasi cha kuukanganya umma.
Nafahamu nabeba dhamana kubwa ya uongozi, taswira yangu ya uongozi daima imeakisi njozi na matumaini ya wananchi wa Kigoma Kaskazini, wananchi wanyonge na vijana kote nchini bila kujali itikadi zao za kisiasa, jinsia zao, makabila yao na rika zao. Hivyo, nawajibika kupitia kwenu kuwatoa hofu juu ya hisia potofu zinazopandikizwa kwao na wale wasiopenda kuona baadhi yetu tukiwaunganisha na kuwasemea watanzania wasio na sauti, dhidi ya vitendo vya hujuma na vyenye dhamira ovu kwa taifa.
Mkakati huo wa kuniunganisha na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaotuhumiwa kwa kupokea Rushwa unatekelezwa kwa njia zifuatazo:
- Kumekuwa na kauli za watendaji wa serikali ambao wamekuwa wakizieneza na hususan kutoa taswira kwamba baadhi ya kauli zangu zinatokana na ushawishi wa rushwa;
- Kuna taarifa ambazo zimeandikwa tena katika kurasa za mbele za baadhi ya vyombo vya habari zikidai ’’Zitto kitanzini’’ ama ’’Zitto sawa na popo nundu’’ zikiashiria kwamba na mimi ni mla rushwa; na
- Waandishi wa habari na jamii kwa ujumla wamefikia kuaminishwa habari hizi kiasi cha wengine kuuliza kwa nini Mhe. Zitto Kabwe hakutajwa katika orodha iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani.
Ndugu Waandishi,
Naomba kutoa ufafanuzi wa hicho kinachoelezwa kwamba nina ushiriki katika masuala ya rushwa hususan kwenye masuala yanayohusu sekta ya Nishati na Madini:-
- Mara baada ya bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Usambazaji wa Umeme Tanzania (TANESCO) chini ya Uenyekiti wake Meja Jenerali Mstaafu Robert Mboma kutangaza kwamba imemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Nd. William Mhando ili kupisha uchunguzi wa baadhi ya vitendo/mwenendo wake, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ambayo mimi ni Mwenyekiti wake ilimuandikia Mhe. Spika kumuomba aridhie ili Kamati iweze kuwaita Bodi ya TANESCO, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG) na pia Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kujiridhisha na tuhuma zote zinazotajwa zinafanyiwa uchunguzi wa kina na hatua kuchukuliwa;
- Kamati ya POAC ninayoiongoza ilimuomba Mhe. Spika kuwaita wahusika tajwa kwa kuwa zilikuwapo tetesi kuwa kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi huyo siku chache kabla ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kulikuwa na lengo la kufunika ’madudu’ makubwa zaidi kwa kulichagiza Bunge na tukio hilo dogo, mkakati ambao naona umefanikiwa sana. Isitoshe, Kamati kutaka kujiridhisha na hatua za Bodi ni sehemu ya msingi ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati yaliyowekwa kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge na pia Shirika la TANESCO ni moja kati ya mashirika ambayo yanawajibika kwetu kwa hesabu zake na pia ufanisi wake kwa ujumla. Tumefanya hivyo pia katika mashirika mengine, hili la TANESCO sio tukio la kipekee;
- Kitendo hiki cha halali na kwa mujibu wa Kanuni kilichofanywa na Kamati yangu kimetafsiriwa kwa makusudi na baadhi ya watu kwamba ni ishara ya kuwa sisi au zaidi kwamba mimi nina maslahi binafsi na TANESCO na hususan Mkurugenzi wake Injinia Mhando, ndio maana tumetaka maelezo ya Bodi. Ukweli kwamba Kamati ya POAC tumewaita pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu (CAG) na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa jambo hilo hilo umefichwa kwa makusudi!
- Baada ya tukio hilo, nikiwa hapa Dodoma, mwandishi wa habari wa gazeti moja alinifuata akiniambia kuwa wamekutana na Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu wake, Nd. Eliachim Maswi hapa hapa Bungeni na wamewaambia kuwa mimi nimepewa rushwa. Hakutaja nimepewa rushwa na nani, kiasi gani na wala kwa lengo gani!
- Nimejaribu kumtafuta kwa simu Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu wake ili wanipe ufafanuzi juu ya mimi na Kamati ya POAC kuhusishwa na tuhuma hizi bila mafanikio, hali ambayo inaniondolea mashaka juu ya ushiriki wao katika kueneza au kuthibitisha uvumi huo. Najaribu sana kujizuia kutokuwa na mashaka na ushiriki wao huo ikizingatiwa uzito na taswira ya nafasi zao katika jamii, lakini wameshindwa kunidhihirishia tofauti.
Sasa naomba kutoa ufafanuzi rasmi kuhusu mlolongo wa matukio hayo tajwa ambayo yanatumiwa na baadhi ya wanasiasa kuonesha kwamba eti nimehusika na vitendo vya rushwa.
- Binafsi sijawahi kuwa na mawasiliano ya aina yeyote na uongozi wa TANESCO kushawishiwa juu ya hatua ambazo POAC ndio imezichukua za kutaka kujiridhisha juu ya utaratibu uliotumika. Ieleweke wazi kabisa kuwa, hakuna wakati wowote, popote ambapo mimi binafsi au Kamati yetu imekataa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO kuchunguzwa kwa tuhuma zozote. Ambacho tumesisitiza wakati wote ni ufuatwaji wa taratibu, kanuni na sheria, hili nitalisimamia iwe masika au kiangazi;
- Ni kwa sababu hiyo, na kwa kujiamini kabisa nimeunga mkono suala la tuhuma za rushwa zinazotajwa zichunguzwe na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kina;
- Nimekwenda mbali zaidi kukiomba chama changu CHADEMA kifanye pia uchunguzi na tathmini yake kwa kina kujiridhisha na tuhuma hizo;
- Natumia fursa hii pia kuomba vyombo vya Dola vichunguze tuhuma hizo kwa nafasi yake ili kuweza kupata ukweli;
- Ninaahidi kushiriki kikamilifu iwapo nitatakiwa katika uchunguzi wowote utakaofanywa na niko tayari kuwajibika iwapo nitakutwa na hatia yeyote.
Napenda niwatoe hofu wananchi wa jimbo la Kigoma Kaskazini walionituma kuja kuwawakilisha hapa Bungeni na Watanzania wote kwa ujumla kwamba:-
- Mimi Zitto Zuberi Kabwe sina bei, sijawahi kuwa nayo na sitarajii kuwa nayo huko mbeleni. Daima nimesimamia kidete maadili ya uongozi bora katika maisha yangu yote ya siasa, na nawaahidi sitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa katika nchi hii pamoja na mikakati ya aina hii ya kunidhoofisha na kunivunja moyo;
- Nafarijika na salam mbali mbali zinazotolewa kunifariji na kusisitiza kuwa nisilegeze kamba katika mapambano haya, nimepokea ujumbe mwingi kwa simu, sms, tweeter na hata facebook na niko pamoja nanyi Watanzania wenzangu kamwe sitarudi nyuma hadi kieleweke. Naamini katika nchi yetu tunazo rasilimali za kutosha mahitaji/haja ya kila mmoja wetu lakini si ‘tamaa/ulafi’ wa baadhi ya watanzania wenzetu;
- Napenda kuweka rekodi sawa kwa Watanzania kwamba nimekuwa Mbunge hiki ni kipindi cha pili, Mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) huu ni takriban mwaka wa saba sasa, Kamati yangu inasimamia mashirika 259 ya Umma na si TANESCO peke yake. Mchango wa Kamati hii katika Bunge na kwa ustawi wa Mashirika ya Umma ni bayana na haujawahi kutiliwa shaka. Kamati yetu imeokoa upotevu mkubwa wa mali za umma na kuokoa fedha za umma kutokana na umakini wake. Tumefanya hivyo CHC hivi karibuni, Kiwira na kwenye mashirika mengine mengi. Kote huko uadilifu na uzalendo wa Kamati hii haujawahi kuhojiwa. Inatuwia vigumu kuona kuwa tunahojiwa katika suala hili la TANESCO. Hapa pana kitendawili.
- Zipo hoja pandikizi za kutaka Kamati ya POAC ivunjwe na haswa zikinilenga mimi binafsi. Nafahamu kiu ya wasioitakia mema nchi yetu kuiona POAC ikivunjwa au sura zikibadilishwa kwa kuwa Kamati hii imekuwa mwiba kwa mikakati yao ya kifisadi. Kwa maoni yangu, Kamati ya POAC isihusishwe na tuhuma hizi kwa vyovyote vile. Niko tayari nihukumiwe mimi kama mimi na sio kuhusisha wajumbe wengine ambao hawatajwi mahala popote katika tuhuma hizi mbaya sana katika historia ya Bunge letu. Nitakuwa tayari kunusuru Kamati ya POAC na maslahi ya taifa letu kwa kujiuzulu Uenyekiti iwapo itathibitika pasipo shaka kuwa nimehongwa. Kamati ya POAC ni muhimu zaidi kuliko mimi.
- Nafahamu pia kuwa kuna wanasiasa hasa wa Upinzani ambao wanautaka sana Uenyekiti wa POAC na wanafanya kila njia kutaka kuidhoofisha. Lakini hawajui kuwa anaepanga wajumbe wa Kamati ni Spika wa Bunge.
- Msishangae pia kuja baadae kubaini kwamba baadhi ya wanasiasa wenye midomo mikubwa ya kutuhumu wenzao wao ndio vinara wa kupokea rushwa.
- Ni lazima tufike mahali kama viongozi kwamba utaratibu unapokiukwa na yeyote yule, au uongo unapotolewa hadharani tuseme bila kuogopa. Hili ndio jukumu letu kama wabunge na viongozi. Kusimamia ufuatiliaji wa utaratibu ni jukumu letu kama Kamati ya POAC na ndio sababu ya msingi ya kuanzishwa kwa mamlaka kama CAG na PPRA. Haiwezekani, tuwe na set ya kanuni kwa kundi fulani na nyingine kwa makundi mengine, au kuhukumu ufuataji wa taratibu kwa kuangalia sura ya mtu usoni
Mwisho
Kumejengeka tabia hivi sasa ya kuwamaliza wanasiasa wenye kudai uwajibikaji na uzalendo. Kumeanzishwa kiwanda kwenye medani ya siasa cha kuzalisha majungu na fitna zenye lengo la kuwachonganisha wanasiasa wa aina hiyo na wananchi kwa kutumia vyombo vya habari na nguvu ya fedha. Naamini mbinu hizi chafu, kama nyingine nyingi zilizojaribiwa kwangu huko nyuma nazo zitashindwa.
Naamini katika kweli na kweli daima huniweka huru. Naamini kuwa mwale mdogo wa mwanga wa mshumaa hufukuza kiza. Kwa imani hiyo, sitasalimu amri mbele ya dhamira zao ovu hata nitakapobaki peke yangu katika mapambano hayo ya kulinda na kutetea rasilimali za taifa zinufaishe watanzania wote.
Daima nitaongozwa na busara ya Hayati Shabaan Robert isemayo, ‘Msema kweli huchukiwa na marafiki zake, nitakapofikwa na ajali hiyo, sitaona wivu juu ya wale wawezao kudumu na marafiki zao siku zote, siwezi kuikana kweli kwa kuchelea upweke wa kitambo, nikajitenga na furaha ya kweli itakayotokea pale uwongo utakapojitenga”.
0 comments:
Post a Comment