Tuesday, August 28, 2012

Waandishi Wetu
SENSA ya Watu na Makazi jana iliingia siku yake ya pili, huku kasoro kadhaa ikiwamo ukosefu wa vifaa, upungufu wa makarani na watu kugoma kuhesabiwa vikiripotiwa.Katika baadhi ya maeneo hadi jana, wananchi walikuwa hawajaanza kuhesabiwa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na ukosefu wa vifaa na makarani.

Ofisa Uhamasishaji wa Sensa Taifa, Said Ameir alikiri kupata taarifa za kasoro hizo lakini akaeleza kushangazwa na chanzo chake, akisema: “Vifaa tulivigawa maeneo mbalimbali nchini kulingana na mahitaji. Tunashangazwa na taarifa hizo kwamba hata wengine wamekosa reflector (makoti ya kuakisi mwanga) na vitambulisho.”

“Tunachofanya sasa ni kuchunguza tatizo hilo limeanzia wapi na limesababishwa na nini. Vilevile tunajitahidi kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vinapelekwa sehemu hizo ili kazi hiyo iendelee kama kawaida.”
Alisema pamoja na kasoro hizo, kazi hiyo inaendelea vizuri na itakamilika ndani ya siku saba kama ilivyopangwa.

Kasoro
Baadhi ya makarani wa Kata ya Ubungo wamesema baadhi ya wajumbe wa nyumba kumi wamekataa kushirikiana nao.
Mratibu Msaidizi wa Sensa kata hiyo, Pertronia Lyamuya alisema tatizo jingine ni baadhi ya waumini wa Kiislamu kugoma kuhesabiwa kama ilivyokuwa kwa baadhi ya wakazi wa Kinondoni Shamba, Dar es Salaam.
Katika baadhi ya maeneo, makarani, walilazimika kutumia polisi kutekeleza majukumu yao. Baadhi ya mitaa ambayo polisi walitumika ni Juhudi, Kingugi na Kiburugwa iliyoko Temeke. Mitaa hiyo ilikuwa imebandikwa matangazo ya kuwahamasisha watu wasishiriki Sensa.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiburugwa, Engerasia Lyimo alisema kazi ya kuhesabu watu ilisimama kwa muda kusubiri polisi wa kuwasindikiza makarani hao kwenye nyumba hizo ili kulinda usalama wao.
Lyimo alisema katika Mtaa wa Kingugi, alijitokeza mjumbe wa shina wa CCM (jina tunalo),ambaye aliwahamasisha wakazi wa eneo lake wasijitokeze kuhesabiwa.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Basihaya, Kinondoni, Daniel Aron alisema kaya nane zilikataa kuhesabiwa kwa maelezo kwamba hazioni umuhimu wake. Alisema baada ya tukio hilo alitoa taarifa Ofisi ya Kata ya Boko.
Alisema kimsingi, changamoto kubwa katika eneo lake ni uchache wa vifaa kiasi cha makarani kushindwa kuanza kazi hiyo.
Msimamizi wa Kata ya Buguruni, Wilaya ya Ilala, Stella Mshana amesema kuwa baadhi ya watu wamekataa kuhesabiwa, wengine kutokana na imani za kidini na wengine kwa kutoelewa umuhimu wake.
“Maeneo ya Mnyamani tumekutana na vikwazo lakini kusema ukweli idadi yao ni ndogo kuliko wanaotupa ushirikiano. Unaweza ukakuta labda katika watu sabini, mmoja ndiye anakataa,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki amesema Serikali itaendelea kupambana na kundi la watu wanaojihusisha na kusambaza ujumbe wa kupinga kushiriki Sensa.

Alisema jana kwamba hadi sasa Polisi inawashikilia watu wanne kutoka Wilaya za Temeke na Kinondoni.... “Kijana mmoja alijulikana kwa jina la Yusuph Ernest alikamatwa akisambaza ujumbe huo maeneo ya Magomeni Kagera.”

Arusha

Watu wasiojulikana, juzi walibandika mabango yanayowazuia makarani wa Sensa kutekeleza wajibu wao katika Kata za Ngarenaro na Unga Ltd. Mabango hayo yalibandikwa katika eneo la Daraja la Ngarenaro.Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo pamoja na Mratibu wa Sensa Mkoa wa Arusha, Magreth Martin walisema hadi jana hakukuwa na tukio la kukwamisha Sensa licha ya kuwapo kwa tukio hilo.

“Nawashukuru sana wananchi wa Arusha kwa kushiriki vyema Sensa katika siku hizi mbili za mwanzo baada ya kuelimishwa na kuelezwa umuhimu wake kwa mipango ya Serikali na maendeleo ya taifa licha kuwapo baadhi ya watu waliojaribu kuwashawishi kususia.”

Tanga

Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Ibrahim Matovu wamewaagiza makarani wa Sensa kwenda kuwahesabu wanawake ambao waume zao wanadaiwa kukimbilia kusikojulikana kukwepa kuhesabiwa.Walitoa amri hiyo baada ya kuripotiwa kuwa baadhi ya Waislamu wa Kijiji cha Kigombe, Muheza, wamekimbilia porini kukwepa kuhesabiwa.

Inadaiwa kuwa baadhi ya wanaume waliondoka na kutoa amri kwa wake zao kutohesabiwa vinginevyo wangepewa talaka.
Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Kigombe, Mashauri Kanyama alisema tatizo hilo limesababisha baadhi ya makarani kushindwa kutekeleza kazi zao kikamilifu.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kigombe, Mohamedi Hatibu alisema baadhi ya wakuu wa kaya wametishia pia kuwapa talaka wake zao iwapo watahesabiwa.


Kilimanjaro
Baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kilimanjaro wamesema Sensa ya Watu na Makazi imekwenda vizuri.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi walilalamika kwamba makarani walikuwa wakisuasua kufanya kazi hiyo.
Walisema makarani wamekuwa wakitumia muda mwingi na kwamba waliotegemea kuhesabiwa Jumapili, hawakuwaona makarani.

“Tulitegemea tutahesabiwa Jumapili na wengi hatukutoka nyumbani tukiwasubiri hasa ikizingatiwa ilikuwa siku ya mapumziko,” alisema Eben Ndosi, Mkazi wa Njiapanda Himo, Wilaya ya Moshi.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mto Mabungo, Wilaya ya Moshi, Estarick Mbuya alisema kazi hiyo ni ngumu lakini itafanikiwa.

Wananchi wa Wilaya ya Hai, Kilimanjaro wamehimizwa kujitokeza kuhesabiwa katika Sensa bila kujali wito wa kutojiandikisha.Msimamizi wa Kata ya Masama Mashariki, katika Kitongoji cha Modio, Mwalimu Bernedicta Kilasara alisema katika taarifa yake kuwa mpaka kufika jana jioni, kaya 320 zilikuwa zimeshahesabiwa nyingi zikiwa za waumini wa Kiislamu.Kilasara alisema Waislamu wa Kitongoji cha Modio walikuwa wakihimizana kujiandikisha.

Igunga walipwa
Wenyeviti  wa vitongoji wilayani Igunga, Tabora wameanza kulipwa posho zao za Sensa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Igunga, Protace Mgayane alisema wenyeviti hao kutolipwa fedha hizo ilikuwa ni moja ya sababu za kutofanikisha kwa kiasi kikubwa kazi hiyo kwani viongozi hao ndiyo wanaofahamu maeneo yao pamoja na jamii ya eneo husika.

Wilaya ya Igunga ina wenyeviti wa vitongoji 632 na kila mmoja atalipwa Sh10,000.
Alisema fedha hizo ni kutoka katika bajeti ya Sensa ambayo imetokana na marekebisho yaliyofanywa katika baadhi ya matumizi ili kuwalipa viongozi hao muhimu wa vitongoji.


Ngorongoro

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali amewataka wakazi wa wilaya hiyo kutowaficha na kuwaandikisha watu kutoka Kenya, katika Sensa ya Watu na Makazi inayoendelea nchi nzima.

Lali alisema wananchi kutoka nchi hiyo jirani wamekuwa na uhusiano na mwingiliano wa kikoo na wakazi wa Ngorongoro hasa wa jamii ya Kimasai na kwamba hawatakiwi kuandikishwa kama Watanzania.
“Naomba kutoa wito kuwa wanaopaswa kuandikishwa ni Watanzania na kama kuna hao wageni kuna taratibu zake na wasiandikishwe kama ni Watanzania,” alisema Lali.

Ngorongoro ni moja ya wilaya za mpakani ambazo watu wake wana uhusiano mkubwa ukiwamo wa kikoo na moja ya koo hizo ni ya Loita ambayo ni ya Wamasai waliopo Kenya na Tanzania.

Watimuliwa Morogoro
Baadhi ya makarani wa Sensa katika Tarafa ya Turiani, Morogoro wamedai kufukuzwa kwenye baadhi ya kaya kwa kutuhumiwa kuwa matapeli kutokana na kukosa fulana na kofia kama Serikali ilivyotangaza kwenye vyombo vya habari.
Tukio hilo lilitokea juzi ambako karibu makarani wote wa Sensa kwenye tarafa hiyo hawakupata sare licha ya kuwa na vitambulisho jambo ambalo baadhi ya wenye kaya walikataa kuwakubali.

Serikali kupitia vyombo vya habari, ilishatangaza kwamba makarani wa Sensa watafika kwenye nyumba wakiwa wamevalia fulana na kofia zilizoandikwa Sensa, mifuko myeusi, lakini makarani wa Turiani hawakutekelezewa hayo.
“Nilifanya kazi ya ziada kumwomba mwenyekiti wa kitongoji ili anisaidie kuwaelimisha kwani walikuwa wanakataa,” alisema karani mmoja wa Kitongoji cha Kigugu.

Alisema changamoto nyingine ni kuchelewa kwa baadhi ya vifaa vya Sensa pamoja na kutumia ramani ya mwaka 2004 ambayo imepitwa na wakati kwani baadhi ya watu waliotajwa kuwamo walishafariki au walishahama.

Habari hii imeandikwa na Patricia Kimelemeta, Pamela Chilongola, Aisha Ngoma, Kelvin Matandiko, Zaina Malongo, Zacharia Osanga, Aziza Masoud, Geofrey Nyang’oro, Dar; Josephine Sanga - Moshi, Mustapha Kapalata - Igunga, Hussein Nyari - Hai, Mussa Juma - Arusha, Mustapha Kapalata - Igunga, Peter Saramba, Arusha, Lauden Mwambona, Turiani.
VIA MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment