Tuesday, July 3, 2012

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, jana iliwasilisha maoni yao kuhusu utendaji kazi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Katika maoni yao, kambi hiyo imeshauri Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Usalama wa Taifa, zifanye kazi ya kuhakikisha usalama unakuwepo badala ya kuwalinda viongozi wa Serikali.

Akiwasilisha maoni hayo kuhusu mapitio na utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/12 na makadirio ya mapato na matumuzi ya ofisi ya Rais kwa mwaka 2012/13, msemaji wa kambi hiyo Profesa Kulikoyela Kahigi, alisema nchi imeingia katika kashfa mbalimbali zinazoruhu rasilimali za nchi kuporwa na viongozi waandamizi serikalini kushiriki mipango ya kuwaibia walipa kodi.

Alisema hawajawahi kusikia Usalama wa Taifa wamehusika kuzuia mchakato huo japo wanakuwa na taarifa za kutosha hivyo kusababisha wananchi kukosa imani na idara hiyo.

Aliongeza kuwa, nchi si salama kwa sasa kwani kitendo cha Wahabeshi kuingia nchini ni ushahidi kuwa usalama wa nchi upo mashakani.

“Usalama wa Taifa na vikosi vyote vya ulinzi na usalama vilikuwa wapi hadi Wahabeshi wakavuka mpaka wetu, kuendelea na safari hadi Kongwa?”

“Kitendo cha kutekwa na kuteswa kiongozi wa madaktari nchini, Dkt. Steven Ulimboka na vyombo vya usalama vipo ni dhahiri kuwa hali ya usalama ni ya mashaka,” alisema Prof. Kahigi na kusisitiza kuwa, upinzani unaitaka Serikali kuunda upya Idara ya Usalama wa Taifa ili iendane na dhana husika ya kulinda masilahi ya nchi na wananchi wake.

0 comments:

Post a Comment