Friday, July 20, 2012

Mbunge wa Kigamboni, Dkt. Faustine Ndugulile, amesema kuwa licha ya kusimamishwa kuhudhuria vikao vitatu Bungeni kwa ajili ya kuwatetea wananchi wa Kigamboni, ataendelea kupambana kuhakikisha haki inatendeka kwa wakazi wa Kigamboni.

Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti la TANZANIA DAIMA, mbunge huyo alisema hapingi kuanzishwa kwa mji mpya wa Kigamboni, bali anapinga taratibu zilizotumiwa na serikali kutekeleza mradi huo.

Alisema suala la uendelezaji wa Mji Mpya unatawaliwa na Sheria ya Mipango Miji Na.8 ya 2007 ambapo sheria hii inaelezea kwa ufasaha taratibu zinazopaswa kuchukuliwa tangu hatua ya kutangaza kwa mradi hadi utengenezaji wa mpango kamili.

Kwa mujibu wa sheria hii, mchakato huu unapaswa kushirikisha wananchi katika kila hatua. Aidha, kifungu 24 (2) kinatamka bayana kuwa Mamlaka ya Kupanga Mji (Planning Authority) inaweza kusimamisha uendelezaji na ujenzi kwenye eneo la mradi kwa kipindi kisichozidi miaka miwili ili kutoa nafasi ya kuandaa mpango kamili.

Akizungumzia hali ilivyo, mbunge huyo alisema takriban miaka minne sasa tangu kutangazwa kwa kusudio la kujenga Mji Mpya wa Kigamboni. Serikali imeshindwa kukamilisha mpango kamili ndani ya miaka miwili kwa mujibu wa sheria.

“Kwa vipindi tofauti, mawaziri na watendaji wa Wizara ya Ardhi, Makazi na Maendeleo ya Nyumba wameshindwa kutoa majibu kamili kuhusu lini mradi huu unaanza; maeneo ambayo mradi utaanzia; viwango vya fidia na hatma ya waathirika wa mradi huu. Vile vile, wananchi hawajashirikishwa kikamilifu katika mchakato wa mradi huu kama Sheria ya Mipango Miji inavyotaka,” alisema Dkt. Ndugulile.

Akizungumzia madhara ya kuchelewa kwa mradi huo, Dkt. Ndugulile alisema umewaathiri kisaikolojia, kiuchumi na kisiasa kwa wakazi wa Kigamboni.

Alizitaja athari hizo kuwa ni pamoja na wananchi kushindwa kujenga na kukarabati nyumba zao, kushindwa kuuza nyumba na ardhi yao na kushindwa kukopesheka kwenye mabenki.

“Manispaa ya Temeke nayo imeathirika katika maeneo yafuatayo. Kushuka kwa mapato ya kodi za majengo, baadhi ya wananchi wameacha kulipa kodi za majengo na vile vile viwango vya tozo za kodi vimepungua baada ya kushuka kwa thamani za nyumba kutokana na uchakavu na kutokarabatiwa,” alisema mbunge huyo.

Katika hatua nyingine Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, amedaiwa kukiuka Kanuni za Kudumu za Bunge kifungu (71) (2) (3) na (4) wakati alipomwadhibu Dkt. Ndugulile, asihudhurie vikao vitatu mfululizo baada ya kushindwa kuthibitisha tuhuma kwamba madiwani wa Halmashauri ya Manispaa Temeke walihongwa ili kuukubali Mradi wa Mji Mpya wa Kigamboni.

Ndugai alitumia kifungu cha 73 (3) ambacho kinampa mamlaka ya kumwadhibu mbunge aliyeshindwa kuthibitisha tuhuma alizozitoa, huku pia akiwa amekaidi kufuta kauli yake kuhusiana na tuhuma hizo.

Baadhi ya wanasheria na wabunge waliozungumza na gazeti hili walisema Ndugai alitumia jazba katika kufikia uamuzi huo na hivyo kukiuka utaratibu mzima wa kanuni za Bunge unaotumika kushughulikia malalamiko ya mtu asiye mbunge.

Ndugai alipaswa kutumia kifungu cha 71(2) na (3) katika kushughulikia sakata hilo la Dkt. Ndugulile na madiwani kwa kuwasilisha malalamiko hayo kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili kuyatafakari na kulishauri Bunge. Adhabu ya mbunge huyo inamalizika leo.

via TanzaniaDaima


0 comments:

Post a Comment