Sunday, July 29, 2012

Mwanafunzi wa darasa la pili jijini Dar es Salaam amefanyiwa unyama wa kutisha na mama yake mzazi kwa kuchanjwa na viwembe mwili mzima na kumsababishia kushindwa kwenda shuleni kutokana na kupata maumivu makali.

NIPASHE Jumapili ilifanikiwa kufika katika eneo la tukio huko Mbezi Temboni mtaa wa Gape na kuzungumza na mwanafunzi huyo wa kiume mwenye umri wa miaka nane aliyesema kuwa mama yake, Jane Maparuwe alimchanja na viwembe maeneo ya mgongoni na kwenye paja juzi majira ya saa 5:00 usiku.
Akisimulia mkasa huo mtoto huyo alisema kuwa alikula maharage baada ya kusikia njaa kwa muda mrefu na mama yake aliporudi nyumbani na kuanza kuulizia yaliyopo maharage hayo, alimwambia kuwa amekula ndipo alipomkamata na kuanza kumpiga na kumchanja na kiwembe.
Alisema mbali na kuchanjwa pia alipigwa kwa kutumia mkanda huku akimkwaruza na kucha zake usoni na kumwachia alama.
Alisema kutokana na kipigigo hicho alishindwe kwenda shuleni kwa kuwa alikuwa na maumivu makali ya mguu na mgongo. Alisema mpaka sasa hapati huduma ya hospitali na kwamba mama yake mdogo alinunua plasta na kumbandika katika kidonda cha mguuni.
Alisema katika kipindi chote amekuwa akiishi na mama yake na kwamba baba yake Nassor Hassan anaishi eneo la Mwananyamala.

Hata hivyo, mtoto huyo amekuwa akiishi maisha ya tabu kwani mama yake huwa anaondoka na kwenda katika biashara zake za kuchoma mihogo na kurudi usiku, huku mtoto huyo akisubiri huruma ya majirani kumpa chakula. "Huwa ninashinda peke yangu mama anakwenda katika biashara zake anarudi saa 3 usiku huwa nakula kwa majirani wakati mwingine ananipa hela ya kununua juisi na skonzi," alisema.
NIPASHE Jumapili ilifanikiwa kuzungumza na Mjumbe wa shina namba nane katika mtaa huo wa Gape, Pendaeli Kahaya, ambaye alisema majira ya saa 6 :15 mchana akiwa katika shughuli zake alipigiwa simu na majirani zake na kumjulisha tukio la mtoto kuchanjwa na viwembe na kisha kufungiwa ndani.
Alisema fundi ujenzi mmoja ambaye huwa anafanya ujenzi katika nyumba hiyo alitaka maji ya kunywa, alipoingia ndani alishangaa kukuta damu zikiwa zimetapakaa na ndipo alipomuuliza mpangaji mwenzake.

"Fundi huyo alijibiwa kuwa kuna mtu alikuwa anakula mali yake alipomuuliza ni kwanini amchanje chanje na kumfungia ndani mpangaji huyo alimjibu hawezi kuelewa ndipo fundi huyo alipokwenda kumuangalia," alisema Kahaya.
Kahaya alisema kabla ya mama huyo kumchanja kwa viwembe alichukua kisu na kumtaka kumchinja mtoto huyo lakini mdogo wake aliingilia kati na kumueleza kuwa ataondoka kama atathubutu kufanya kitendo hicho.
Alisema mdogo wake aliondoka na ndipo mama wa mtoto huyo alipoamua kumuagiza mtoto wa jirani kwenda kununua viwembe na kuamua kumchanja na kumfungia ndani kwa siku mzima.
Hata hivyo, alisema wakati mtoto huyo akifanyiwa tukio hilo jirani yake aliamka na kumuuliza ni kwanini anampiga mtoto huyo kwa muda mrefu lakini mama huyo alimtukana jirani huyo na kumtaka afuatilie mambo yake na sio ya kwake.

Alisema tukio hilo lilimsikitisha na kuamua kwenda kumjulisha diwani wa kata ya Msigani, Rogati Mbowe, na kumwambia aende kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa serikali za mtaa.
Aidha, alisema aliwasiliana na uongozi wa serikali za mtaa ambao ulichukua hatua juu ya suala hilo na askari walifika katika eneo hilo na kufanikiwa kumkamata mama huyo.
Alisema wameshangazwa kuona mtoto huyo mpaka sasa hajapelekwa hospitali na pia mama huyo ameshaachiwa na polisi jambo ambalo limewashtua wakazi wa eneo hilo.

"Sijaelewa sababu ambayo polisi imepelekea mama huyo kuachiliwa tunataka kuona sheria inachukua mkondo wake maana nilijiuliza maswali mengi hivi ni mtoto wake aliyemzaa kwa kumbebea mimba ya miezi tisa na kuamua kumchanja na viwembe," alisema. NIPASHE ilifanikiwa kuzungumza na diwani Mbowe ambapo alisema kuwa ni kweli tukio hilo limetokea na kwamba kesho atalifuatilia kwa ukaribu kwani alikuwa amepata majukumu mengine.

NIPASHE ilimtafuta mama mzazi wa mtoto huyo katika sehemu yake ya biashara eneo la Kimara Temboni lakini wafanyabishara wenzake walidai kuwa alikuwa ameshaondoka katika biashara zake na kuelekea nyumbani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo hakuweza kupatikana.
Hata hivyo, habari za ndani ambazo limelifikia gazeti hilo ni kwamba polisi wameagizwa kumkamata mama huyo ambaye aliachiwa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

0 comments:

Post a Comment