PANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO) KWA MWAKA 2012/2013
(Kanuni ya 99(7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Mwaka huu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetimiza miaka arobaini na
nane tangu kuzaliwa kwake baada ya Rais wa Jamhuri ya Tanganyika Mwalimu
Nyerere kutia saini Makubaliano ya Muungano na Rais wa Jamhuri ya Watu
wa Zanzibar Sheikh Abedi Amani Karume tarehe 22 Aprili, 1964.
Wakati anawasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha
2011/2012, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano)
aliliambia Bunge lako tukufu kwamba “… katika kipindi hicho Muungano
wetu umekuwa na mafanikio katika maeneo ya kijamii, kiuchumi na
kisiasa…. Muungano wetu ndio nguzo kuu ya umoja na amani.”
Hata
hivyo, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri aliliambia Bunge lako tukufu
kwamba, licha ya mafanikio hayo, “… zipo changamoto katika kumaliza
vikwazo vinavyokwamisha shughuli za Muungano.” Mheshimiwa Waziri
hakuzitaja changamoto hizo.
‘MAPITO’ YA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Katika Utangulizi wake kwa Chapisho la Pili la Mhadhara wa Kiprofesa
(Professorial Inaugural Lecture) uliotolewa Januari 1990 na Profesa Issa
G. Shivji na kupewa kichwa cha Tanzania: The Legal Foundations of the
Union, Profesa Yash Ghai – aliyekuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam wa kwanza kutoka Afrika Mashariki – anasema
kwamba kwa kuzingatia mazingira ya kuanzishwa kwa Muungano na historia
yake, “… kitu cha ajabu sio kwamba umekuwa na matatizo, bali ni kwamba
umedumu (licha ya matatizo hayo) – na kwenda kinyume na mwelekeo katika
Afrika.”
Muungano ulidumu misuguano ya miaka ya mwanzo kati ya
Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume iliyohusu kuongezwa kwa masuala ya
fedha na sarafu katika orodha ya Mambo ya Muungano. Aidha, Muungano
ulidumu mauaji ya viongozi waandamizi na wajumbe wa Baraza la Mapinduzi
la kwanza la Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kama Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Watu wa Zanzibar Abdallah Kassim Hanga, Waziri wa Fedha Abdul Aziz
Twala, Othman Sharrif, Mdungi Ussi, Saleh Saadalla na wengine wengi.
Vile vile, Muungano ulidumu mauaji ya Sheikh Karume mwenyewe mwaka
1972; ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa’ Zanzibar iliyopelekea
kung’olewa madarakani kwa Rais Aboud Jumbe mwaka 1984; alichokiita
Mwalimu Nyerere ‘udhaifu’ wa Rais Mwinyi; na kifo cha Mwalimu Nyerere
mwaka 1999.
Kwa bahati mbaya, Mheshimiwa Spika, ‘mapito’ haya
ya Muungano yamekuwa yanafichwa fichwa, licha ya kauli za mara kwa mara
za ‘kuelimisha umma juu ya Muungano.’ Kwa sababu hiyo, zaidi ya tendo la
kuchanganya udongo na matukio mengine yaliyofanyika hadharani, historia
halisi ya Muungano wetu haifahamiki kwa wananchi walio wengi. Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba wakati umefika sasa kwa
Serikali kuweka wazi nyaraka mbali mbali zinazohusu historia ya Muungano
wetu na ‘mapito’ yake ili Watanzania waelewe masuala yote yaliyotokea
yanayouhusu.
Hii ni muhimu zaidi kwa kuzingatia ukweli kwamba
mataifa ya magharibi kama vile Marekani na Uingereza yalikwishatoa
hadharani nyaraka za mashirika yao ya kijasusi pamoja na balozi zao za
Tanzania zinazoonyesha jinsi ambavyo serikali za mataifa hayo zilihusika
katika kuzaliwa kwa Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Kuanikwa kwa nyaraka zilizoko katika mamlaka mbali mbali za Serikali
kutasaidia kuthibitisha au kukanusha taarifa ambazo chanzo chake ni
nyaraka za kidiplomasia na kijasusi za nchi hizo kwamba Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ulitokana na njama za kibeberu za kudhibiti
ushawishi wa siasa za kimapinduzi za Chama cha Umma na viongozi wake
ndani ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar la wakati huo.
Aidha,
nyaraka hizo zitatoa mwanga juu ya kilichowasibu viongozi waandamizi wa
chama hicho ambao bila uwepo wao kutambuliwa rasmi, historia ya
Mapinduzi ya Zanzibar na ya Muungano inabaki pungufu. Kwa maoni ya Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, miaka karibu hamsini ya Muungano ni umri wa
kutosha kwa taifa la Tanzania kuambiwa ukweli wote juu ya kuzaliwa kwake
na mapito ambayo limepitia katika kipindi hicho.
UKIUKWAJI MAKUBALIANO/SHERIA YA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Makubaliano ya Muungano ya tarehe 22 Aprili 1964 yalikuwa ni mkataba wa
kimataifa kati ya nchi mbili huru zilizokubaliana kuunda ‘nchi moja
huru’, kwa mujibu wa ibara ya (i) ya Hati ya Muungano. Ili kutekeleza
Makubaliano ya Muungano, Bunge la Jamhuri ya Tanganyika lilitunga Sheria
ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, 1964, Sura ya 557 ya Sheria za
Tanzania. Kifungu cha 4 cha Sheria hiyo kilitangaza kuunganishwa kwa
Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuwa ‘Jamhuri
moja huru itakayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’
Kwa upande wa Zanzibar, Baraza la Mapinduzi – ambalo ndio lilikuwa
‘Bunge’ la Zanzibar wakati huo – halikutunga sheria ya kuridhia
Makubaliano ya Muungano. Jambo hili limekuwa chanzo cha mjadala mkali
katika duru za kitaaluma na kisheria juu ya uhalali wa Muungano wenyewe.
Kwa vyovyote vile, matokeo ya kusainiwa Makubaliano ya Muungano ni
kwamba Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zilikufa na
nchi moja – iliyokuja baadae kuitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania –
kuzaliwa.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa aya ya (iv)
ya Makubaliano ya Muungano na kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Muungano,
Mambo ya Muungano yaliyokubaliwa kwenye Makubaliano ya Muungano yalikuwa
kumi na moja. Haya ni mambo yaliyoko katika vipengele vya 1 hadi 11 vya
Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Muungano. Hata hivyo, kati ya mwaka
1964 and 1973 mambo mengine sita – yanayoonekana katika vipengele 12
hadi 16 vya Nyongeza ya Kwanza – yaliongezwa katika orodha ya Mambo ya
Muungano.
Hivyo basi, mwaka 1965 masuala ya fedha, sarafu na
benki yaliongezwa; mwaka 1967 leseni ya viwanda na takwimu, elimu ya juu
na mambo yaliyokuwa katika Nyongeza ya X ya Mkataba wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki yaliongezwa; mwaka 1968 yaliongezwa mambo ya maliasili
ya mafuta, petroli na gesi asilia; na mwaka 1973 mambo yanayohusu Baraza
la Mitihani la Taifa yaliongezwa.
Aidha, Mheshimiwa Spika,
Mabadiliko ya Tano ya Katiba ya mwaka 1984 yaligawa kipengele cha
Nyongeza ya X ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutengeneza
vipengele vinne vinavyojitegemea katika orodha ya Mambo ya Muungano,
yaani usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti, utabiri wa hali ya hewa
na takwimu.
Vile vile, Mabadiliko hayo yaliongeza kitu kipya
katika orodha ya Mambo ya Muungano: Mahakama ya Rufani ya Tanzania.
Aidha, kipengele cha 3, yaani ulinzi, kilifanyiwa marekebisho na kuwa
‘ulinzi na usalama.’ Na mwaka 1992 ‘uandikishwaji wa vyama vya siasa’
nao uliongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Mambo yote yaliyoongezwa katika orodha ya Mambo ya Muungano baada ya
mwaka 1964 yalikuwa nje ya Makubaliano ya Muungano na nje ya Sheria ya
Muungano na kwa hiyo yalikuwa batili. Hii ni kwa sababu Sheria ya
Muungano – na sio Katiba za Muda za 1964 au 1965 au ya sasa – ndio
Sheria Mama iliyozaa Muungano na kuweka mgawanyo wa madaraka kati ya
mamlaka za Jamhuri ya Muungano na mamlaka za Zanzibar. Sheria ya
Muungano ilitungwa na Bunge la Katiba tofauti na sheria za kawaida.
Aidha, Katiba ya Muda, 1965 iliyotawala Tanzania hadi 1977 iliiweka
Sheria hiyo kama Nyongeza ya Pili katika Katiba na kuweka masharti
kwamba Sheria hiyo haiwezi kurekebishwa bila marekebisho hayo kuungwa
mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote wa Tanganyika na wale wa
Zanzibar. Vile vile, Katiba ya Muunganoinataja, katika Orodha ya Kwanza
ya Nyongeza ya Pili, kwamba moja ya Sheria ambazo mabadiliko yake
yahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote ni “Sura ya 557
(Toleo la 1965), Sheria ya Kuthibitisha Mapatano ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964.”
Mambo yote haya,
Mheshimiwa Spika, yanaifanya Sheria ya Muungano kuwa na haiba ya Katiba.
Kama alivyosema Profesa Issa Shivji katika The Legal Foundations of the
Union: “Kila mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa sheria amefundishwa
kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapatikana katika
waraka unaoitwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977. Lakini,
nachelea kusema, kila mwanafunzi amefundishwa visivyo.
Katiba
ya Tanzania inapatikana sio katika waraka mmoja, bali katika nyaraka
mbili. Sheria ya Muungano, Sura ya 557 ya Sheria za Tanzania na Sheria
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…. Vivyo hivyo, Katiba ya
Zanzibar inapatikana katika (1) Sheria ya Muungano na (2) Katiba ya
Zanzibar, 1984.” Katika masuala yanayohusu Muungano, kwa mujibu wa
Profesa Shivji, waraka unaotawala ni Sheria ya Muungano.
Hii
ndio kusema kwamba panapotokea mgongano kati ya Katiba au Katiba ya
Zanzibar na Sheria ya Muungano, ni Sheria ya Muungano ndio inayokuwa na
Katiba au Katiba ya Zanzibar inakuwa batili kwa kiasi cha ukiukaji wake
wa Sheria ya Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Kifungu cha 5
cha Sheria ya Muungano, ambacho ndicho chenye misingi mikuu ya Muungano
hakijawahi kurekebishwa tangu Sheria yenyewe ilipotungwa mwaka 1964.
Badala yake, Bunge limekuwa na tabia ya kukwepa kuigusa kabisa Sheria ya
Muungano na badala yake limekuwa likifanya marekebisho ya orodha ya
Mambo ya Muungano iliyowekwa kwa mara ya kwanza katika Katiba za Muda za
mwaka 1964 na 1965 kwa kuongeza vipengele katika orodha hiyo. Lengo la
marekebisho haya, Mheshimiwa Spika, limekuwa mara zote ni kuinyang’anya
Zanzibar mamlaka yake chini ya Sheria ya Muungano.
Ndio maana
katika Mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya CCM Kuhusu Marekebisho ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Katiba ya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar yaliyotolewa tarehe 27 Januari, 1983, CCM ilitamka kwamba “…
msingi wa kuwa na orodha ya mambo ya muungano katika Katiba ni kuonyesha
mamlaka ya Serikali ya Zanzibar ambayo yalikabidhiwa kwa Serikali ya
Muungano; na msingi wa kuongeza mambo zaidi katika orodha ya mambo ya
muungano, kama ambavyo imefanyika mara kwa mara, ni kuhamisha mamlaka
zaidi ya Serikali ya Zanzibar kwenda kwa Serikali ya Muungano.”
Mheshimiwa Spika,
Profesa Shivji anasema – katika The Legal Foundations of the Union –
kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano halikupewa mamlaka ya kuongeza Mambo
ya Muungano bali lilipewa mamlaka ya kutunga sheria zinazohusu Mambo ya
Muungano kama yalivyofafanuliwa katika Sheria ya Muungano. Kwa maana
hiyo, nyongeza zote zilizofanyika katika orodha ya Mambo ya Muungano
tangu mwaka 1964 zilikiuka Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano
na ni batili. Ndio maana, kwa muda mrefu, Wazanzibari wamelalamikia
masuala haya, hasa hasa masuala ya fedha, sarafu na mafuta na gesi
asilia.
Mheshimiwa Spika,
Vitendo vya kupuuza
Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano iliyoridhia Makubaliano
vilifikia kilele chake tarehe 21 Novemba, 2000 pale Mahakama ya Rufani
ya Tanzania ilipotamka – katika kesi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
dhidi ya Machano Khamis Ali na Wenzake 17 – kwamba Zanzibar sio nchi na
wala sio dola. Bali, kwa mujibu wa Mahakama ya Rufani, ‘hakuna ubishi wa
aina yoyote kwamba Jamhuri ya Muungano ni nchi moja na dola moja.’
Kama tulivyokwisha kuonyesha, suala la Mahakama ya Rufani ya Tanzania
yenyewe kuwa suala la Muungano liliingizwa kwenye orodha ya Mambo ya
Muungano kinyemela na kinyume na Makubaliano ya Muungano na Sheria ya
Muungano. Jibu la Wazanzibari juu ya ukiukwaji wa muda mrefu wa
Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano iliyoridhia Makubaliano
hayo lilikuwa ni kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya
Zanzibar mwaka 2010.
KATIBA YA MUAFAKA AU KATIBA YA UHURU?
Mheshimiwa Spika,
Misukosuko ambayo imeukumba Muungano wetu tangu mwaka 1964 hailingani
na hatari kubwa inayoukabili hivi sasa. Kama tulivyomweleza Rais Kikwete
katika waraka wetu wa tarehe 27 Novemba, 2011, “Muungano wetu upo
katika hatari kubwa ya kuvunjika kwa sababu ya mabadiliko makubwa ya
kikatiba ambayo yamefanyika katika Katiba ya Zanzibar, 1984 na kutokana
na Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Hii ni kwa sababu
Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba, 2010, inaashiria tafsiri mpya
ya Makubaliano ya Muungano na ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambayo inahoji misingi ya Jamhuri ya Muungano kama nchi moja,
mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, na mambo muhimu ya Muungano….”
Ili kufahamu jambo hili vizuri, ni muhimu kuelewa kwa undani yaliyomo
katika Sheria hiyo ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 13 Agosti, 2010, wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano likiwa
limevunjwa kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar lilipitisha Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya
Katiba ya Zanzibar, 1984. Mabadiliko haya yaliweka msingi wa kikatiba wa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar inayoshirikisha CCM na Chama
cha Wananchi (CUF). Kwa sababu hiyo, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
imepigiwa upatu kama Katiba ya Muafaka na, kwa kiasi fulani, hii ni
kweli.
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba imekwenda mbali zaidi. Sheria hii sio tu imehoji uhalali wa
orodha ya Mambo ya Muungano ya tangu mwaka 1964 na nyongeza zake
zilizofuata, bali pia imehoji pia misingi muhimu ya Sheria ya Muungano
iliyoridhia Makubaliano ya Muungano. Kwa mtazamo huu, Katiba ya sasa ya
Zanzibar inaelekea kuwa ni tangazo la uhuru wa Zanzibar zaidi kuliko
waraka wa muafaka kati ya vyama viwili vilivyokuwa mahasimu.
Mheshimiwa Spika,
Aya ya (i) ya Makubaliano ya Muungano na kifungu cha 4 cha Sheria ya
Muungano vilitangaza muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya
Watu wa Zanzibar na kuundwa kwa ‘Jamhuri moja huru itakayoitwa Jamhuri
ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’
Huu ndio msingi wa
maneno ya ibara ya 1 ya Katiba ya Muungano kwamba ‘Tanzania ni nchi moja
na ni Jamhuri ya Muungano.’ Na huu ndio ulikuwa msingi wa maneno ya
ibara ya 1 ya Katiba ya Zanzibar ya kabla ya Mabadiliko ya 2010 kwamba
‘Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano.’ Sasa msingi huu wa Muungano
umehojiwa na maneno ya ibara ya 2 ya Katiba mpya ya Zanzibar
yanayotamka kwamba ‘Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.’
Mheshimiwa Spika,
Ibara ya 2(2) ya Katiba ya Muungano inampa Rais wa Jamhuri ya Muungano –
kwa kushauriana kwanza na Rais wa Zanzibar – mamlaka ya kuigawa
Tanzania Zanzibar katika mikoa, wilaya au maeneo mengineyo. Vile vile,
ibara ya 61(3) ya Katiba ya Muungano inampa Rais wa Zanzibar mamlaka ya
kuteua Wakuu wa Mikoa katika Tanzania Zanzibar ‘baada ya kushauriana na
Rais.’ Masuala ya mgawanyo wa nchi katika mikoa na mamlaka za mikoa hiyo
sio, na hayajawahi kuwa, Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Sheria ya
Muungano.
Vile vile hayapo katika orodha ya Mambo ya Muungano.
Ni wazi kwa hiyo, kwamba ibara za 2(2) na 61(3) za Katiba ya Muungano
zilikuwa zinakiuka matakwa ya Sheria ya Muungano na kwa hiyo ni batili.
Sasa wazanzibari ‘wamejitangazia uhuru’ kwa kutangaza – katika ibara ya
2A ya Katiba mpya ya Zanzibar – kwamba “… Rais (wa Zanzibar) aweza
kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata
utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.”
Aidha, kwa ibara ya 61(1), Rais wa Zanzibar hawajibiki tena kushauriana
na Rais wa Muungano pale anapofanya uteuzi wa wakuu wa mikoa ya
Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Wakati ambapo Sheria ya
Muungano ilikuwa imetambua na kuhifadhi mamlaka ya Rais wa Zanzibar kama
mkuu wa dola ya Zanzibar, Mahakama ya Rufani ya Tanzania – katika Kesi
ya Machano Khamis Ali na Wenzake – ilitishia moja kwa moja msingi huo
kwa kutamka kwamba Zanzibar sio nchi na wala sio dola na kwa hiyo
haiwezi kutishiwa na kosa la uhaini.
Sasa ibara ya 26(1) ya
Katiba mpya Zanzibar ‘imerudisha’ dola ya Zanzibar kwa kutamka kwamba
“kutakuwa na Rais wa Zanzibar ambaye atakuwa Mkuu wa Nchi ya Zanzibar,
Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi.” Aidha, kwa kutambua kwamba ‘Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya
Muungano’ sio moja ya Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Sheria ya
Muungano, Katiba ya sasa ya Zanzibar imetamka kwamba katika kesi
zinazohusu ‘kinga za haki za lazima, wajibu na uhuru wa mtu binafsi’,
uamuzi wa majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Zanzibar “… utakuwa ni wa
mwisho na hautokatiwa rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.”
Mheshimiwa Spika,
Kifungu cha 5(1)(a)(iii) na (iv) cha Sheria ya Muungano kinataja
‘ulinzi’ na ‘polisi’ kama sehemu ya mambo kumi na moja ya Muungano. Na
hivyo ndivyo inavyosema aya ya (iv)(c) na (d) ya Makubaliano ya
Muungano. Ijapokuwa ‘ulinzi’ ulichakachuliwa baadae kwa kuongezwa maneno
‘na usalama’, bado ni sahihi kusema kwamba masuala ya ulinzi na polisi
ni masuala halali ambayo Sheria ya Muungano iliyakasimu kwa Serikali ya
Muungano.
Na kwa sababu hiyo, ni sahihi kwa Katiba ya Muungano
kutamka – kama inavyofanya katika ibara ya 33(2) – kwamba ‘Rais (wa
Jamhuri ya Muungano) atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri
Jeshi Mkuu.’
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, katika kile
kinachoonekana kama hojaji kubwa ya msingi huu wa Makubaliano ya
Muungano na Sheria ya Muungano, ibara ya 121 ya Katiba ya sasa ya
Zanzibar imeunda majeshi ya Zanzibar inayoyaita ‘Idara Maalum.’
Majeshi haya, kwa mujibu wa ibara ya 121(2) ni Jeshi la Kujenga Uchumi
(JKU); Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM); Chuo cha Mafunzo (cha
wahalifu), na Idara Maalum nyingine yoyote ambayo Rais wa Zanzibar
anaweza kuianzisha ‘ikiwa ataona inafaa….’ Kuthibitisha kwamba Idara
Maalum ni majeshi, ibara ya 121(4) inakataza watumishi wa Idara Maalum
‘… kujishughulisha na mambo ya siasa….’ Makatazo haya hayatofautiani na
makatazo ya wanajeshi kujiunga na vyama vya siasa yaliyoko katika ibara
ya 147(3) ya Katiba ya Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Sio
tu kwamba Katiba mpya ya Zanzibar inaanzisha majeshi bali pia inamfanya
Rais wa Zanzibar kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi hayo. Kwa mujibu wa
ibara ya 123(1) ya Katiba hiyo, “Rais atakuwa Kamanda Mkuu wa Idara
Maalum na atakuwa na uwezo wa kufanya chochote kile anachohisi, kwa
maslahi ya Taifa (la Zanzibar), kinafaa.” Aidha, kwa mujibu wa ibara ya
123(2), mamlaka ya Rais wa Zanzibar chini ya ibara ndogo ya (1)
yanaingiza “… uwezo wa kutoa amri ya kufanya shughuli yoyote
inayohusiana na Idara hiyo kwa manufaa ya Taifa.”
Kwa maoni ya
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, haya ni mamlaka ya kutangaza au
kuendesha vita ambayo, kwa mujibu wa ibara ya 44(1) ya Katiba ya
Muungano, ni mamlaka pekee ya Rais wa Jamhuri ya Muungano. Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge
hili tukufu kama tafsiri hii ya ibara ya 123 ya Katiba mpya ya Zanzibar
ni sahihi.
Na kama ni sahihi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali itoe tamko Bungeni ni kwa nini imeiruhusu Zanzibar kujinyakulia
mamlaka juu ya mambo ya ulinzi na usalama ambayo kwa historia yote ya
Muungano yamekuwa ni mamlaka pekee ya Serikali ya Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Kifungu cha 5(1)(b) cha Sheria ya Muungano kilitamka kwamba muundo wa
Serikali ya Zanzibar utakuwa kama utakavyoamuliwa na sheria za Zanzibar
pekee. Na hivyo ndivyo ilivyokubaliwa katika aya ya (iii)(a) ya
Makubaliano ya Muungano. Hata hivyo, licha ya muundo wa Serikali ya
Zanzibar kutokuwepo katika orodha ya Mambo ya Muungano, Katiba ya
Muungano imetenga Sura ya Nne nzima kuzungumzia ‘Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la
Zanzibar.’
Kwa mujibu wa Profesa Shivji katika The Legal
Foundations of the Union, Sura ya Nne ya Katiba ya Muungano “… haina
ulazima wowote na ni kuingilia, bila kualikwa, kwenye mambo ambayo yako
ndani ya mamlaka pekee ya Zanzibar.” Ndio maana Katiba mpya ya Zanzibar –
kwa usahihi kabisa – imefanya mabadiliko katika muundo wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar bila ya kuzingatia matakwa ya Sura ya Nne ya Katiba
ya Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Katiba mpya ya Zanzibar
sio tu kwamba ‘imetangaza uhuru’ wa Zanzibar kwa kuhoji misingi muhimu
ya Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano,
bali pia imehakikisha kwamba uhuru huo utalindwa dhidi ya tishio lolote
la Serikali ya Muungano. Hii imefanywa kwa kuweka utaratibu wa kuwepo
kura ya maoni ya wananchi wa Zanzibar kuhusu mabadiliko ya vifungu
kadhaa vya Katiba ya Zanzibar. Kwa mujibu wa ibara ya 80A(1) ya Katiba
hiyo, “… Baraza la Wawakilishi halitaweza kufanya mabadiliko ya Katiba
kuhusiana na sharti lolote lililomo katika kifungu chochote
kilichoainishwa katika kijifungu cha (2) cha kifungu hiki, mpaka kwanza
mabadiliko hayo yakubaliwe na wananchi kwa kura ya maoni.”
Vifungu vinavyohitaji kura ya maoni ni vifungu vyote vya Sehemu ya
Kwanza ya Sura ya Kwanza inayohusu Zanzibar kama nchi na/au dola;
kifungu cha 9 kinachohusu Serikali na watu wa Zanzibar; vifungu vyote
vya Sura ya Tatu inayohusu kinga ya haki za lazima, wajibu na uhuru wa
mtu binafsi; na kifungu cha 26 kinachohusu Rais wa Zanzibar na mamlaka
yake.
Vifungu vingine ni pamoja na kifungu cha 28 kinachohusu
muda wa urais; Sehemu ya Pili na ya Tatu ya Sura ya Nne zinazohusu
Makamu wawili wa Rais, Baraza la Mawaziri na Baraza la Mapinduzi;
kifungu cha 80A kinachohifadhi haki ya kura ya maoni; na vifungu vya 121
na 123 vinavyohusu Idara Maalum na mambo yanayohusiana nayo.
Mheshimiwa Spika,
Kuweka masharti ya kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya vifungu tajwa vya
Katiba mpya ya Zanzibar kuna athari ya moja kwa moja kwa uhai wa
Muungano wetu. Hii ni kwa sababu hata vifungu ambavyo tumeonyesha kwamba
vinakiuka misingi mikuu ya Makubaliano ya Muungano na Sheria ya
Muungano haviwezi kubadilishwa bila kura ya maoni ya Wazanzibari.
Kwa maneno mengine, kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, masuala
ya kama Tanzania ni nchi moja au la, majeshi ya ulinzi, polisi, n.k.
ambayo yamekuwa Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano
na Sheria ya Muungano sio Mambo ya Muungano tena hadi hapo wananchi wa
Zanzibar watakapoamua – kwa kura ya maoni – kuyarudisha kwa mamlaka ya
Muungano. Huku, Mheshimiwa Spika, ni kutangaza uhuru wa Zanzibar bila
kutaja neno uhuru! Huku ni kuua Muungano bila kukiri hadharani!
Mheshimiwa Spika,
Kwa mtazamo wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, hatuna tena nchi moja
inayozungumzwa katika Katiba ya Muungano bali tuna nchi mbili. Kwa
mtazamo huo huo, masuala ya ulinzi na usalama, polisi, n.k. sio tena
Mambo ya Muungano kwa sababu sasa kila nchi ina majeshi yake na kila
moja ina Amiri Jeshi Mkuu wake. Aidha, tuna marais wawili, wakuu wa nchi
wawili viongozi wa serikali wawili. Haya yote yanakiuka moja kwa moja
Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya Muungano.
Kwa upande mwingine, kwa mtazamo wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, Rais wa
Muungano hana tena mamlaka ya kugawa mikoa na wilaya kwa upande wa
Zanzibar, na wala hawezi kumshauri tena Rais wa Zanzibar anapoteua Wakuu
wa Mikoa wa Tanzania Zanzibar. Aidha, Mahakama ya Rufani ya Tanzania –
licha ya kuwa moja ya Mambo ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya Muungano
– haina tena mamlaka ya kusikiliza na kuamua rufaa zinazohusu haki za
msingi na uhuru wa mtu binafsi zinazotoka Zanzibar. Yote haya hayapo
katika Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano lakini yapo katika
Katiba ya Muungano.
KURUDISHWA KWA SERIKALI YA TANGANYIKA
Mheshimiwa Spika,
Katika maoni yetu kuhusu Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilionyesha jinsi ambavyo “tafsiri hii
mpya ya Makubaliano ya Muungano na Katiba ya Jamhuri ya Muungano
imetiliwa nguvu kubwa na Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
ambayo imeipa Zanzibar nafasi na ushawishi mkubwa katika utungaji wa
Katiba Mpya.”
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilionyesha
kwamba, kwa mujibu wa Sheria hiyo, “Rais wa Zanzibar sio tu kwamba ana
mamlaka karibu sawa na Rais wa Jamhuri ya Muungano bali pia ana kura ya
turufu katika mchakato mzima wa Katiba Mpya.” Aidha, tulithibitisha
jinsi ambavyo “… ushawishi mkubwa wa Zanzibar hauishii katika kura ya
turufu aliyo nayo Rais wa Zanzibar pekee yake (bali) Zanzibar ina
ushawishi mkubwa vile vile kutokana na nafasi kubwa iliyo nayo katika
vyombo vingine vinavyoundwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba….”
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia tena tahadhari iliyoitoa
wakati huo kwamba: “Masharti haya ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yana
athari kubwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu yanakiuka
Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, Katiba ya sasa ya Jamhuri ya
Muungano na hata Katiba ya sasa ya Zanzibar….” Na kama tulivyosema
wakati huo, “… tafsiri hii mpya ya Makubaliano ya Muungano na ya Katiba
ya Jamhuri ya Muungano inarudisha mezani mjadala juu ya muundo wa
Muungano wetu na nafasi ya iliyokuwa Tanganyika katika Muungano huo.”
Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyo kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba katika mazingira ambayo upande
mmoja wa Muungano umejitangazia uhuru kama ambavyo tumeonyesha hapa,
huu ni wakati muafaka kuanzishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika.
Katika mazingira ambayo upande mmoja wa Muungano sio tu una Serikali
kamili, Bunge kamili, Mahakama kamili, wimbo wa taifa, bendera ya taifa,
na sasa una nchi kamili yenye mipaka na eneo la bahari linalojulikana,
una majeshi yake na Amiri Jeshi Mkuu wake, huu ni muda mzuri kwa
Serikali ya Tanganyika kuzaliwa upya. Katika mazingira kama haya,
Mheshimiwa Spika, upande wa pili wa Muungano unatakiwa kuwa na vitu
vyote hivyo pia ili uweze kujadiliana na upande wa kwanza katika hali ya
usawa.
Huu ni wakati wa kurudishwa tena kwa Serikali ya
Tanganyika kama ilivyopendekezwa na Tume ya Rais ya Chama Kimoja au
Vyama vingi mwaka 1991 na Tume ya Kissanga mwaka 1998, na kama
ilivyopendekezwa na Kundi la Wabunge 55 wa Bunge hili tukufu na kuungwa
mkono na Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi kabla ya hoja hiyo
kutunguliwa na Baba wa Taifa mwaka 1993!
KURA YA MAONI JUU YA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua kwamba Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba inaielekeza Tume ya Katiba kuongozwa na misingi mikuu ya
kitaifa ya kuhifadhi na kudumisha ‘kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano.’ Hata
hivyo, baada ya kujitokeza kwa wananchi wanaopinga kuendelea kuwepo kwa
Jamhuri ya Muungano, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji
Joseph Sinde Warioba amesema kwamba wale wanaopinga Muungano nao
wajitokeze kutoa maoni yao kwa Tume.
Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inataka Serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili tukufu ni namna
gani maoni ya wale wanaotaka kiini macho hiki cha Muungano kiishe
yatashughulikiwa na Tume ambayo imepewa jukumu kisheria la kukihifadhi
na kukidumisha kiini macho hicho? Ni kipi kitakachoizuia Tume ya Warioba
kupuuza maoni ya watu hao kwa hoja kwamba Sheria inaielekeza Tume
kuratibu na kukusanya maoni na kutoa mapendekezo ya kuhifadhi na
kudumisha Muungano?
Mheshimiwa Spika,
Katika miezi ya
karibuni kumejitokeza makundi ya wananchi, hasa kwa upande wa Zanzibar,
ambayo yamedai kwamba iitishwe kura ya maoni ya wananchi ili kuamua kama
bado kuna haja ya kuendelea na Muungano. Makundi haya, yakiongozwa na
kundi la Uamsho, yameshambuliwa sana hadharani kwa kudaiwa kwamba
yanataka kuvunja Muungano. Na watu ambao wameongoza mashambulizi dhidi
ya wana-Uamsho ni viongozi waandamizi wa CCM, wakiwemo viongozi wakuu
wastaafu wa chama hicho.
Mheshimiwa Spika,
Katika
maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Muswada wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba tulisema kwamba “… hofu … ya kuwaudhi ‘Wazanzibari’
ndio imepelekea kimya kikuu – ndani ya CCM na ndani ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano – juu ya ukiukwaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano uliofanywa na Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya
Zanzibar, 2010.” Naomba nikiri kwamba tulikosea kusema hivyo.
Tulichotakiwa kusema wakati ule, na tunachokisema sasa, ni kwamba kimya
kikuu ndani ya CCM na ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya
ukiukwaji mkubwa wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano pamoja
na Katiba kinatokana sio tu na ‘hofu’ ya kuwaudhi Wazanzibari bali pia
kinatokana na ukweli kwamba viongozi waandamizi wa CCM pamoja na wa
Serikali yake walishiriki katika ukiukwaji huo!
Wao ndio
wanaoongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ndio waliondaa Muswada
wa Sheria ya Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar. Na wao ndio
wanaoongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano waliokula kiapo cha
kuihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Na kwa
hiyo wao ndio walioiruhusu Zanzibar kutangaza uhuru kwa Mabadiliko haya
ya Katiba yake.
Mheshimiwa Spika,
Kwa viongozi hawa na
chama chao kuibuka sasa na kuwatuhumu wana-Uamsho na makundi mengine
kwamba wanataka kuvunja Muungano kwa kudai kura ya maoni ya wananchi
wakati wao wenyewe wamekaa na kupitisha marekebisho ya Katiba ambayo
tayari yamevunja Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba
ya Muungano ni kilele cha juu cha unafiki wa kisiasa. Mashabiki hawa wa
Muungano waeleze walikuwa wapi wakati Zanzibar inatangaza uhuru wake kwa
kuchanachana Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba ya
Muungano.
Mheshimiwa Spika,
Kwa wale wanaodai kwamba
wana-Uamsho wanataka kuvunja Muungano kwa sababu tu ya kudai kura ya
maoni, tunaomba tuwakumbushe yafuatayo. Kwanza, kwa mujibu wa Baba wa
Taifa katika kitabu chake Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania: “Huko
nyuma baadhi ya viongozi wa Zanzibar wapinzani wa Muungano wamewahi
kudai tufanye referendum kwa Zanzibar kuhusu Muungano. Tukakataa kwa
sababu safi kabisa.”
Hapa Mwalimu alikuwa anamzungumzia
aliyekuwa Rais wa Zanzibar Alhaj Aboud Jumbe, Waziri Kiongozi Ramadhani
Haji Faki na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Bashir Ebassuah Kwaw Swanzy
waliong’olewa madarakani mwaka 1984 baada ya ‘kuchafuka kwa hali ya hewa
ya kisiasa.’
Aidha, Mheshimiwa Spika, katika kitabu hicho
hicho Mwalimu Nyerere anasema yafuatayo juu ya kilichotokea kwenye Bunge
hili hili wakati wa Bunge la bajeti la mwaka 1993: “Tarehe 30 Julai,
1993 wakati wa mkutano wa bunge la bajeti ukiendelea, zaidi ya wabunge
50 kwa pamoja walitoa taarifa ya kusudio la kuwasilisha hoja Bungeni
ambayo inadai (kwamba) kuendelea na mfumo huu wa Muungano usiowaridhisha
wananchi wengi wa upande mmoja ni kuhatarisha kuendelea kudumu kwa
Muungano….
Hivyo basi wabunge hawa wanaliomba Bunge … liazimie
kwamba Serikali … ilete Muswada Bungeni kabla ya Februari 1994,
kurekebisha katiba ya Jamhuri ya Muungano ili kuwezesha uundaji wa
‘Serikali ya Tanganyika’ ndani ya Muungano…. Tarehe 20 Agosti, 1993
wabunge wahusika waliwasilisha taarifa nyingine … iliyokuwa inalitaka
Bunge … liazimie kwamba Serikali … iandae kura ya maoni ambayo
itafanyika kabla ya 31 Desemba, 1994 ili kupata maoni ya wananchi wa
Tanzania juu ya kuundwa kwa “Serikali ya Tanganyika” ndani ya Muundo wa
Muungano….”
Pili, Mheshimiwa Spika, Katiba ya sasa ya Zanzibar
ambayo mashabiki wa Muungano wameileta kwa kupitia Sheria ya Mabadiliko
ya Kumi ya Katiba tayari imewapa wananchi wa Zanzibar haki ya kuamua,
kwa kura ya maoni, mambo mbali mbali yanayoihusu nchi hiyo na namna
itakavyoongozwa. Mashabiki hawa wa Muungano wakubali kuvuna
walichopanda, wasibeze wale wote wanaotaka kutumia haki ya kura ya maoni
kuamua hatma ya Muungano na nafasi ya Zanzibar ndani au nje yake.
Mheshimiwa Spika,
Ni wazi, kwa kuzingatia ushahidi huu, kwamba madai ya kuwa na kura ya
maoni ya wananchi ili kuamua masuala makubwa yanayohusu Muungano wetu ni
ya siku nyingi na yametolewa na watu na taasisi mbali mbali. Madai haya
hayajaanzishwa na wana-Uamsho wala CHADEMA. Ni wazi vile vile kwamba
kura ya maoni inaruhusiwa kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Zanzibar.
Kwa sababu hizi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaungana na wale wote
ambao wamedai, na wanaendelea kudai kuitishwa kura ya maoni ya wananchi
ili waweze kuamua mustakbala wa nchi yetu. Kuendelea na kiini macho cha
Muungano wakati Serikali zote mbili na chama tawala cha CCM wanauvunja
kivitendo kutaipelekea nchi yetu kwenye njia ya Ethiopia na Eritrea, au
Sudan na Sudan Kusini au Yugoslavia ya zamani.
Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inataka Watanzania waamue, kwa kura ya maoni, kama bado
wanataka kuendelea na Muungano na kama jibu lao ni ndio, ni muundo gani
wa Muungano wanautaka. Kama, kwa busara zao, wataamua kwamba nusu karne
ya Muungano inatosha basi itakuwa afadhali kwenda njia ya
Czechoslovakia ya zamani kuliko kwenda njia ya Yugoslavia ya zamani, au
Ethiopia na Eritrea au Sudan na Sudan Kusini.
Mwisho,
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali
iwaeleze Watanzania juu ya hatua, kama zipo, ilizozichukua kuzuia
ukiukwaji huu wa Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba.
Na mwisho, Serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili tukufu kama – kwa
ukiukwaji huu wa Makubaliano ya Muungano, Sheria ya Muungano na Katiba
ya Muungano – Bunge hili tukufu litakuwa ndani ya mamlaka yake kuchukua
hatua za kumshtaki Rais kwa mujibu wa ibara ya 46A ya Katiba kwa
kushindwa kuihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Muungano kama kiapo
cha kazi yake kinavyomtaka.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wajumbe wote wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni chini ya uongozi wa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni Mheshimiwa Freeman A. Mbowe kwa ushauri na ushirikiano
uliowezesha maandalizi ya maoni haya. Aidha, niwashukuru familia yangu –
mke wangu mpenzi Alicia Bosensera na mapacha wetu Agostino Lissu na
Edward Bulali – kwa kuendelea kuvumilia upweke unaotokana na ‘Daddy’
kuwa mbali muda mwingi kwa sababu ya majukumu mazito ya kibunge.
Aidha, niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Singida Mashariki kwa
imani na nguvu wanayonipa kila siku kwa kuendeleza msimamo wetu thabiti
wa kukataa kunyanyaswa, kunyonywa na kupuuzwa na ‘Ndaa ya Njou’! Mwisho
naomba nichukue fursa hii kuwashukuru viongozi, wanachama na wapenzi
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wananchi wote wa Tanzania
ambao wameendelea kutuunga mkono na kututia nguvu katika kipindi hiki
muhimu katika historia ya nchi yetu. Ninawaomba waendelee kutuunga mkono
na kututia nguvu katika siku ngumu na za majaribu makubwa zinazokuja!
Mheshimiwa Spika,
Baada ya maelezo haya marefu, naomba kukushukuru na wewe binafsi na naomba kuwasilisha.
—————————————————————
Tundu Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO)
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
0 comments:
Post a Comment