Mwenyekiti mpya wa Yanga, Yusuf Manji.
Na Saleh AllyKWA mara ya kwanza, Mwenyekiti mpya wa Yanga, Yusuf Manji, amezungumzia kipigo cha mabao 5-0 ambacho timu yake ilikipata kutoka kwa watani wao, Simba, kabla ya yeye kuingia madarakani.
Simba ambao ni mabingwa wa Tanzania Bara, waliitandika Yanga kwa mabao 5-0 katika mechi ya mwisho ya kufunga msimu iliyochezwa Mei 6, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na Championi Ijumaa katika mahojiano maalum, Manji alisema kipigo hicho kiliisambaratisha Yanga na ndicho kilichangia yeye kugombea nafasi hiyo na akasisitiza inawezekana kulipa kisasi.
“Kilikuwa kipigo kibaya na kilitusambaratisha, ilikuwa ni aibu, ndiyo maana uongozi wangu utafanya kazi kubwa ya kurudisha imani kwa Wanayanga. Hicho ni kitu muhimu sana.
“Hatuwezi kuacha kuizungumzia Simba kwa kuwa ni changamoto kwetu, kinachotakiwa kwa Yanga ni kuangalia mipango madhubuti ambayo siku ya mwisho itatufanya tuwe na timu imara.
“Kama tuna timu imara, kuifunga Simba au timu yoyote mabao tano, hakitakuwa kitu kigumu. Kujipanga kwa mipango na programu za uhakika, ndiyo kitu bora kuliko kukimbilia kulipa kisasi tu,” alisema akionyesha kujiamini.
Manji alisisitiza kuwa wachezaji lazima wajue wana jukumu kubwa la kurejesha heshima ya Yanga na kocha atahusika katika kuhakikisha kikosi chake kinafanya kweli.
“Kama viongozi, tutahakikisha mishahara, posho au kama kuna ahadi, kila kitu kinapatikana kwa wakati mwafaka. Sasa wachezaji na makocha wahakikishe tunafanya vizuri. Tunajua timu haiwezi kujengwa kwa siku mbili. Hatuwezi kutimiza ahadi zetu kwenda katika mafanikio kama tutakuwa na timu inayofungwa,” alisema Manji.
Kikosi cha Yanga kwa sasa kipo chini ya Kocha Mbelgiji, Tom Saintfiet na kimeanza michuano ya Kagame kwa kufungwa mabao 2-0 na Atletico ya Burundi kabla ya kuibuka na kuinyonya ‘damu’ Wau Salaam ya Sudan Kusini kwa mabao 7-1.
0 comments:
Post a Comment