Wednesday, July 4, 2012

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania Dkt. Steven Ulimboka ameombewa ulinzi kwenye Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International.

Vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka ndani ya jopo la wataalam na jumuia hiyo kwa nyakati tofauti vimeliambia Tanzania Daima Jumatano kwamba wamelazimika kuomba ulinzi wa kimataifa ili kukabiliana na watu wabaya wanaotaka kumdhuru.

Vyanzo hivyo vilisema watu waliomdhuru wanataka kummaliza kabisa ili kuficha ukweli kwani kabla ya kuondoka Dk. Ulimboka alieleza ukweli wa tukio hilo hivyo wabaya wake hao wanatumia baadhi ya watumishi wa ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kuhakikisha wanampata.

“Hii ya kuomba ulinzi ni ‘latest’; Amnesty International ni wabishi lakini katika hili wameombwa naamini watakubali kumlinda… maombi yamepelekwa jana.

“Kabla ya kupelekwa Afrika Kusini Dk.t Ulimboka alieleza ukweli wa tukio zima kuanzia walivyomkamata na mateso waliyompa hadi walipotaka kumzika akiwa hai.

“Wameshajulikana sasa wanatumia ubalozi wetu kutaka kupenya kwenda kumwona hospitalini ndiyo maana haisemwi yuko hospitali gani… ukweli ni kwamba usalama wa Dkt. Ulimboka uko hatarini,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika.

Bila kujua kwamba hizo ni habari chanzo hicho kiliendelea kueleza kuwa, akiwa njiani kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dkt. Ulimboka aliwataka viongozi na madaktari wengine ndani ya jumuia kupigania haki zao.

Kwa mujibu wa chanzo hicho mwenyekiti huyo wa jumuia aliwasihi waliobaki wasikubali damu yake imwagike bure, wahakikishe maslahi ya madaktari yanaboreshwa.

“Msikubali damu yangu imwagike bure; endeleeni kupigania haki zenu…,” chanzo hicho kilimnukuu Dk. Ulimboka.

Hata hivyo ilielezwa kwamba jumuia hiyo ilishirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binaadam (LHRC) kuomba ulinzi huo kutoka Amnesty International.

Juhudi za gazeti hili kumpata Mkurugenzi Mtendajiwa LHRC Hellen Kijobi-Simba ziligonga mwamba baada ya kuzungumza na ofisa wa kituo hicho aliyetambulika kwa jina la Rose Mwalongo.

Mazungumzo kati ya Rose na Tanzania Daima Jumatano yalikua hivi:

Tanzania Daima Jumatano: Haloo! Samahani naomba namba ya mama Kijo Bisimba nina shida naye.

Rose: Haloo! Subiri kidogo nitakupa.

Tanzania Daima Jumatano: Asante dada Rose.

Baada ya dakika tatu ofisa huyo wa LHRC alipiga tena simu na mambo yakawa hivi:

Tanzania Daima Jumatano: Haloo dada Rose!

Rose: Haloo! Mama amepumzika hataki kupokea simu kwani kuna ishu gani kama naweza kukusaidia.

Tanzania Daima Jumatano: Ni ishu ya kiofisi kwamba LHRC imemsaidia Dkt. Ulimboka kuomba ulinzi kutoka Amnesty International naomba kujua ukweli wa habari hiyo.

Rose: Sikia. Siyo kila kitu kinatakiwa kupelekwa kwenye 'media' kwa mtu kama huyu unaposema kila kitu unaweza kumsababishia matatizo lakini sidhani kama atajibu kuhusu suala hilo.

Alisema ofisa huyo na kukata simu.

0 comments:

Post a Comment