Wednesday, June 20, 2012

ASEMA HATA WANAOTAKA KUUVUNJA WALETE MAONI YAO YATASIKILIZWA  
Na Ayoub Mangi 
MWENYEKITI wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao hata kama ni ya kutaka kuvunja Muungano katika mchakato wa kuundwa kwa Katiba mpya.  Kauli hiyo ya Jaji Warioba imekuja kipindi ambacho kuna vuguvugu la kutaka Zanzibar ijitenge, linalofanywa na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam (JUMIK), na kusababisha machafuko visiwano humo.

Jana, Jaji Warioba akizungumza na waandishi wa habari kutangaza kuanza rasmi kazi kwa tume hiyo tangu ilipozinduliwa rasmi April 13, mwaka huu, aliweka wazi msimamo huo unaoondoa mkanganyiko katika suala hilo.  Kumekuwapo sintofahamu kuhusu msimamo wa Serikali juu ya Muungano, hasa baada ya Rais Jakaya Kikwete kueleza suala hilo kama moja ya tunu za Taifa, ambayo haitakiwi kujadiliwa kwa lengo la kuuvunja. Jaji Warioba alifafanua kwamba, tume hiyo inafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kwamba itakusanya maoni yote na kuyaratibu, ili kupata Katiba wanayoitaka wananchi wenyewe. 

“Tume inafanya kazi kwa kufuata sheria. Na kwa kuwa klatika mchakato ni lazima tuanze na Katiba ya sasa, kwanza wananchi waseme upungufu wake. Wananchi wako huru kupendekeza, kwa mfano, kuwepo kwa Serikali yaani Bunge na Mahakama, labda wanataka tuwe na Rais dikteta, waseme,” alisema Jaji Warioba na kuongeza: “Kuhusu Muungano, tutayapokea maoni yote. Kama wanataka mambo ya Muungano yapunguzwe, au yaongezwe, Serikali moja au mbili au wanataka tuvunje Muungano, yote tutayapokea. Tusiseme watu wamezuiwa, hakuna aliyezuiwa.”          

Akifafanua kifungu cha tisa cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inayotumika katika mchakato huo, Jaji Warioba alisema Katiba haiwezi kuundwa kama hakuna nchi, ndiyo maana, suala la Muungano limewekwa kuwa la msingi.  Kifungu hicho kinazungumzia mambo ya msingi (tunu za taifa), ambayo Tume ya Katiba itayazingatia wakati wa kukusanya maoni ya wananchi.  “Muswada wa kwanza uliyataja hayo mambo ya msingi kama matakatifu, lakini marekebisho yaliyofuatia yalibadilisha na kuweka kuwa mambo ya msingi. Tume inayazingatia kwa sababu huwezi kuunda Katiba kama hakuna nchi.

Katiba tuliyonayo inasema Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano,” alifafanua Jaji Warioba. Kuhusu tume hiyo kufanya kazi Zanzibar kabla Sheria ya Mabadiliko ya Katiba haijaridhiwa na Baraza la Wawakilishi, Jaji Warioba alisema Katiba ya Zanzibar haisemi hivyo, badala yake inaelekeza kutoa taarifa tu.  “Utaratibu uliopo ni sheria kuwekwa mezani, ndivyo ilivyo. Sheria zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano zinatakiwa ziwekwe mezani, Baraza haliendi kujadili bali linapewa tu taarifa,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:,  “Sheria hii ilitungwa Novemba mwaka jana na Baraza limekutana Januari mwaka huu.

Kwa utaratibu wa kawaida ilitakiwa iwekwe mezani kwenye Baraza mwezi huo, lakini kukawa na marekebisho mwezi Februari, baada ya hapo tukaipeleka. Sisi tume wala hatuna wasiwasi kwa sababu hilo limeshapita.” Kifungu cha 132 (1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kinasema:

 “Hakuna sheria yoyote itakayopitishwa na Bunge la Muungano ambayo itatumika Zanzibar mpaka Sheria hiyo iwe ni kwa ajili ya mambo ya muungano tu na ipitishwe kulingana na maelekezo yaliyo chini ya vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Na kifungu cha 132 (2) kinasema, “ Sheria kama hiyo lazima ipelekwe mbele ya baraza la Wawakilishi na Waziri anayehusika.”

Uratibu wa maoni
Kuhusu  uratibu wa maoni ya Katiba, Jaji Warioba alitaja maeneo manne muhimu yaliyopewa uzito katika ukusanyaji wa maoni kuwa ni misingi ya Taifa ambayo ni uhuru, haki, udugu, amani, demokrasia na Serikali kutofungamana na dini yoyote, ingawa wananchi wake wana uhuru wa kuabudu, huku eneo la pili likiwa ni mamlaka ya wananchi.

“Kuna watu wanasema mamlaka ya wananchi hayakufafanuliwa kama vile Serikali, Bunge na Mahakama, tume ingependa kusikia maoni ya wakulima, wafanyakazi, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wanaume, wanawake, wazee, vijana na walemavu,” alisema.   Aliyataja maeneo mengine kuwa ni malengo muhimu na msingi ya mwelekeo wa shughuli za Serikali, kama inavyoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya tisa na eneo la Haki za Binadamu na wajibu wa jamii, kama inavyoelezwa katika sehemu ya tatu ya Katiba.

Marupurupu ya Tume/ Utaratibu
Akizungumzia madai kwamba wajumbe wa tume hiyo wanalipwa marupurupu mengi, Jaji Warioba japo hakufafanua mishahara ya wajumbe alisema hizo ni tetesi zisizo na ukweli.

“Nimesikia ‘speculations’ (tetesi) nyingi kuhusu hayo. Lakini, ninyi mtubane kwa kazi tuliyopewa ya kukusanya maoni….Hapa kuna wengine wana mapato ya chini kuliko huko walikokuwa, kwa kuwa tu wanaona umuhimu wa kulitumikia taifa lao… Sijui kila mtu analipwa kiasi gani…,” alisema Jaji Warioba. Akizungumzia utaratibu wa kazi wa tume hiyo, Jaji Warioba alisema kuwa tume hiyo itaanza kazi katika mikoa minane ya Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga.

Aliongeza kuwa tume hiyo itakuwa na nyaraka mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu ya Katiba kwa wananchi, ikiwa ni pamoja nakala 500,000 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano, nakala 10,000 za Katiba ya Zanzibar na nakala 500,000 za Sheria ya Katiba ya mwaka 2012.  Alisema baada ya kukusanya maoni hayo, Tume itakutana na mabaraza ya Katiba na mwishowe rasimu ya Katiba itafikishwa kwenye Bunge Maalum.  Aliwataka waandishi wa habari kuwaelimisha wananchi ili waone umuhimu wa kushiriki katika mchakato huo.

Vurugu za JUMIK
Hivi karibuni visiwa vya Zanzibar na viunga vyake vilikumbwa na vurugu kubwa baada ya kundi la Uamsho kufanya vurugu na kutaka visiwa hivyo vijitenge kuwa dola huru. Hata hivyo, vurugu hizo zilidhibitiwa na Jeshi la Polisi, lakini juzi zililipuka upya na polisi kulazima tena kutumia nguvu kuzidhibiti.  Ends  

0 comments:

Post a Comment