WIZARA ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, imesema kuwa
umasikini uliokithiri miongoni mwa jamii ni moja ya chanzo cha wimbi
kubwa la watoto wa mitaani.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana, Elisante ole Gabriel,
alitoa kauli hiyo juzi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika
iliyoandaliwa na Shirika la Hope for the Children Organization.
Akizungumza kwa niaba yake, ofisa mwandamizi wa idara hiyo, Focas
Kapinga, alisema jamii inapaswa kutambua kuwa jukumu la kuwalea watoto
hao ni la Watanzania wote.
Kwamba umasikini umekuwa ukichangia hali hiyo ya watoto wa mitaani
kutokana na baadhi ya wazazi kushindwa kuzihudumia familia zao ipasavyo,
matokeo yake watoto huamua kukimbilia mitaani kwa matumaini ya kupata
maisha bora.
Kapinga alisema kuvunjika kwa ndoa kumekuwa kukisababisha familia
kushindwa kukidhi mahitaji muhimu kwa watoto, kama vile elimu, chakula,
mavazi hali inayowalazimisha kuondoka majumbani kwao.
Alibainisha kuwa, wizara hiyo ndiyo yenye jukumu la maendeleo ya
vijana, wakiwemo watoto, na kwamba dhamira yao ni kukabiliana na mambo
yanayosababisha watoto kukimbilia mitaani.
“Wizara imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika
ya kimataifa kama vile UNICEF, ILO, UNEPA, UNDP na ya watu binafsi
yaliyoko nchini na taasisi za dini katika kutimiza azma yake,” alisema.
Kapinga alibainisha kuwa, jitihada hizo ni pamoja na utoaji wa elimu
ya ujasiriamali, stadi za maisha na mikopo kwa vijana yenye masharti
nafuu.
Awali Mkurugenzi wa Hope for the Children Organization, Joyce Mang’o,
alisema pamoja na mipango mingi ya serikali, lakini bado imekuwa ikitoa
mchango hafifu wa kupambana na tatizo hilo.
Alisema sheria zilizopo hazilengi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa
asasi na watoto pia, jambo linalosababisha asasi kuwa na utendaji hafifu
usiokidhi haja na matakwa kwa wahusika.
0 comments:
Post a Comment