Thursday, June 7, 2012


Maoni ya katuni
Serikali ilipitisha sera ya kuwapatia matibabu ya bure wazee, wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kutokana na makundi hayo kutokuwa na uwezo.

Kwa mujibu wa sera hiyo ya mwaka 1990 pamoja na marekebisho ya mwaka 2009, wazee wote wenye umri wa kuanzia miaka 60, wajawazito  na watoto chini ya miaka mitano wanatakiwa kutibiwa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali zote za serikali bila gharama yoyote.

Hata hivyo, utekelezaji wa sera hiyo umekuwa mgumu kiasi kwamba makundi haya yanashindwa kupata huduma za bure. Katika toleo la jana la gazeti hili tulichapisha ripoti maalum ikielezea malalamiko ya wazee katika mikoa mbalimbali ya Tanzania kuhusiana na kushindwa kupata matibabu bure.

Wazee hao wameeleza mambo mengi yanayowakwaza kupata matibabu bure. Wanalalamika kwamba hospitali wanazokwenda kutibiwa hazina dawa na kwamba wanaandikiwa dawa waende kuzinunua kwa fedha zao katika maduka ya dawa.

Wanalalamika kuwa licha ya kuwepo kwa madirisha maalum ya matibabu ya bure kwa wazee, wanajikuta wakitumia muda mrefu katika foleni kutokana na uchache wa watoa huduma.

Pia wazee wanalalamikia urasimu katika baadhi ya hospitali, vituo vya afya na zahanati kwamba wanasumbuliwa kwenda kupata huduma wakiwa na barua kutoka kwa watendaji wa vijiji na kata, ambazo zinawatambulisha kuwa ni wazee wasio na uwezo.

Kadhalika, baadhi wanasema kuwa wanacheleweshewa kufanyiwa vipimo kama vya X-Ray na Ultrasound kutokana na urasimu wa watoa huduma.

Hata hivyo, baadhi ya menejimenti za hospitali wamekiri kwamba wazee wanalazimika kujinunulia dawa na mapungufu mengine katika utoaji wa huduma kwa kada hiyo.

Kwa mfano, viongozi wa hospitali hizo wanasema kuwa, tatizo kubwa linalowalazimisha madaktari na watoa huduma wengine kuwaandikia wazee dawa za kwenda kununua linasababishwa na ufinyu wa bajeti ambalo wanapangiwa, hali ambayo inawakwaza kumudu kununua dawa nyingine wanazozihitaji wazee ambazo ni za gharama kubwa.

Kwa upande wake, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inasema kuwa, miongoni mwa mambo yanayochangia huduma mbovu za matibabu kwa wazee ni wahudumu wengi katika hospitali za umma kutofahamu kwa undani huduma ya bure ya matibabu kwa wazee, kina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

Tumesikitishwa na kushangazwa na huduma mbovu za matibabu kwa wazee licha ya serikali kutunga na kuipitisha sera ya kuwapa matibabu bure wazee na makundi mengine kutokana na kutambua kuwa hayo ni makundi ambayo hayana uwezo wa kugharamia matibabu.

Sababu zilizotolewa na serikali kutokana na kukwama kwa utekelezaji wa sera hiyo hazina ushawishi na kinachoonekana ni kukosekana kwa utashi wa serikali. Kama serikali ingekuwa na utashi, bila shaka suala hilo lingepewa kipaumbele.

Haiingii akilini kumwandikia mgonjwa mzee dawa ili aende kuzinunua mwenyewe wakati ikijulikana kuwa mhusika hana uwezo wa kumudu kuzinunua dawa hizo na kumfanyia hivyo ni sawa na kumkejeli.

Wazee ni watu ambao kila uchao wanahitaji kwenda kupata matibabu kwa kuwa mtu anapokuwa mzee huandamwa na magonjwa mengi yanayotokana na uzee, hivyo ni vigumu kwao kumudu kujinunulia dawa hizo. Isitoshe, sio wazee wote ambao wana watoto au ndugu wenye uwezo wa kiuchumi wa kuwasaidia kugharamia huduma za matibabu.

Kwa hiyo, serikali inawajibika kuongeza bajeti katika hospitali za umma na kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kuwa huduma za bure za matibabu kwa wazee, wajawazito na watoto zinapatikana na zenye ubora.

Urasimu wa kuwataka wazee kwenda kupata matibabu wakiwa na barua za watendaji wa vijiji na kata unaweza kuondolewa kwa kuwasajili wazee wote ambao hawana uwezo na kuwapatia vitambulisho maalum ili watambuliwe na hospitali za umma kwamba wanastahili kutibiwa bure.

Utaratibu huo utawawezesha wazee kwenda kupata tiba wakati wowote wanaohitaji huduma hiyo, badala ya kwenda kuandikiwa barua wakati amezidiwa.

Ni matumaini yetu kuwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii itatekeleza ahadi yake kwa kuweka mkakati wa kuzungukia hospitali na utoaji ushauri kwa hospitali hizo.

0 comments:

Post a Comment