Monday, June 4, 2012

















 Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe anakabiliwa na mtihani wa kwanza baada ya wajumbe wa Kamati ya Miundombinu kukataa kuipitisha bajeti yake wakitaka maelezo ya bajeti iliyopita kutekelezwa chini ya asilimia 40.

Dk Mwakyembe alipandishwa kutoka Naibu Waziri wa Ujenzi kuwa Waziri wa Uchukuzi katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete Mei 4 mwaka huu.

Wizara hiyo mpya inagusa sekta nyeti za miundombinu ya kiuchumi na kijamii ikiwamo usafiri wa anga, reli, bandari, huku bajeti yake ikitajwa kutokidhi mahitaji ya shughuli za wizara.

Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya kamati hiyo zinaeleza katika kikao cha juzi, baadhi ya wajumbe walisema hawawezi kupitisha bajeti hiyo mpaka wapate maelezo kutoka kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuhusu kutokutekelezwa kwa bajeti ya 2011/2012 ili wajue bajeti ijayo itatekelezwa vipi.

Chanzo cha habari ndani ya kamati hiyo kilifafanua kwamba wakati baadhi ya wajumbe akiwamo, Anne Kilango Malecela wakipinga, Mwenyekiti wa Kamati, Peter Serukamba alikuwa akishinikiza ipitishwe na kamati jinsi ilivyo, akisema badala yake wangeenda kuipinga bajeti kuu ya Serikali.

Hata hivyo, licha ya Serukamba kujaribu kutumia nafasi ya kiti chake kushinikiza bajeti hiyo ipitishwe, bado mpango huo uligonga ukuta baada ya Kilango ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo na wenzake kuendelea kupinga.

Upande huo wa wajumbe wanaopinga mpango huo umekuwa ukieleza wasiwasi wao juu ya utekelezwaji wa bajeti mpya wakati ile ya awali haijatekelezwa hata nusu yake.

Taarifa hizo ziliongeza kwamba, msimamo wa wanaopinga ni kutaka kukutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kuachana na utaratibu kama uliofanywa katika bajeti ya mwaka 2011/12, ambayo Serikali ililazimika kunusuru baadhi ya bajeti za wizara katikati ya mkutano wa Bunge.

Katika bajeti ya mwaka jana, Serikali ililazimika kufanya mipango ya dharura kuokoa baadhi ya bajeti ikiwamo ya Nishati na Madini, ambayo wabunge waliikataa wakisema, haikuwa ikionyesha namna ya kutatua matatizo ya umeme ndipo Serikali ikatangaza kutenga Sh1.2 trilioni kwa mpango wa dharura kuanzia Agosti mwaka jana hadi Desemba mwakani.

Kukwepa mipango hiyo ya dharura, baadhi ya wajumbe waliopinga walisisitiza, “Tunataka tukutane na Waziri Mkuu kwanza tujue kwa nini bajeti iliyopita haijatekelezwa yote badala yake Serikali imetoa fedha chini ya asilimia 40?  Tuna wasiwasi kwamba hii mpya pia haitatekelezwa, hatuwezi kuipitisha bajeti hiyo.”

Chanzo chetu kilisema, “Kulitokea mvutano baada ya Serukamba kusema, hakuna haja ya kukataa bajeti hiyo bali waende wakaikatae bajeti ya Serikali ili ipate fundisho.”

Baada ya kauli hiyo, Kilango alisimama na kuhoji kuwa mwenyekiti anataka kuiangusha Serikali na kumtaka aeleze anachokifanya ni kitu gani, kwani bajeti isipopita Serikali itaanguka na haitafanya kazi," kiliongeza chanzo hicho.

Hata hivyo, pamoja na mvutano huo chanzo chetu kimeeleza kuwa Serukamba aliendelea kusisitiza hilo na aliamua kumhoji Dk Mwakyembe kama wameridhika na bajeti hiyo, naye hakujibu ndiyo wala hapana, bali alisema wizara yake inahitaji fedha.

Kutokana na baadhi ya wajumbe kusimamia msimamo huo wa kutoipitisha bajeti hiyo bila kupata maelezo ya Pinda, Serukamba alikubali kuwa wengi wapewe na kukubaliana nao wasubiri hadi  maelezo ya serikalini yatolewe.

Chanzo chetu kilieleza wakati hayo yakitokea, Dk Mwakwembe na Naibu wake, Dk Charles Tizeba walikuwamo pamoja na viongozi wa taasisi mbalimbali ambazo ziko chini ya wizara hiyo.

Kauli ya Serukamba
Alipopigiwa simu Serukamba kuhusu taarifa hizo, alikanusha na kudai hawajaigomea bajeti hiyo, wataipitisha.

“Hizo taarifa si za ukweli, kwanza sikupaswa kuongea na chombo cha habari. Hizo taarifa usiandike kwani nitatoa taarifa kesho (leo),” alisema Serukamba na kuongeza;

“Kesho (leo) tutakutana na wizara tena, lakini nisikilize hizo taarifa si za kweli, ila nitaongea na waandishi wa habari kesho (leo). Tutaipitisha ila kuna maelezo tunayahitaji kutoka serikalini.”

Kwa upande wake Kilango, alipoulizwa alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa halihusiani na waandishi wa habari, bali ni la kamati na kuongeza kwa kung'aka, “Siwezi kuzungumza na vyombo vya habari.”

Kwa upande wake Dk Mwakyembe jana alipoulizwa kuhusu utekelezaji huo wa bajeti kwa kiwango cha asilimia 40 katika bajeti iliyopita na kwamba alijiandaje kukabili changamoto hiyo, alisema amejipanga vizuri kubaliana na hali hiyo.

"Tumejipanga vizuri kubalina na hilo," alisema kwa kifupi Dk Mwakyembe.

Hata hivyo, taarifa ambazo Mwananchi ilizipata baadaye zilisema, Dk Mwakyembe kwa sehemu kubwa ya siku ya jana alikuwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, huku taarifa zikisema suala hilo la utata wa bajeti ndiyo ilikuwa mada kuu.
 Boniface Meena kutoka MWANCHI GAZETI

0 comments:

Post a Comment