Saturday, June 23, 2012

 na Grace Macha, Arusha
ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Arusha, Rafael Mbunda (51), Mwanasheria wa halmashauri hiyo, Paul Mugasha, kaimu mweka hazina, Christopher Mbarakai na mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Luneco, Nestory Ng’hoboko, wamefikishwa mahakamani kwa makosa ya uhujumu uchumi ikiwemo kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya sh milioni 25.5.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Gwantwa Mwanguga, washtakiwa hao walisomewa makosa manne tofauti na waendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na 

Rushwa Nchini (TAKUKURU), Hangi Chang’a na Rehema Mteta.
Shtaka la kwanza la matumizi mabaya ya madaraka linawakabili Mbunda, Mbarakai na Mugasha ambapo wanadaiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kumwezesha mkurugenzi wa kampuni ya Luneco Investment, Ng’hoboko, kuwasilisha nyaraka za zabuni bila kufuata sheria ya manunuzi ya umma nchini.
Mteta alidai mahakamani hapo kuwa shtaka la pili linalowakabili washtakiwa hao watatu wanaodaiwa kuwa Agosti 23, 2010, washtakiwa hao waliokuwa watumishi wa halmashauri hiyo walitoa zabuni ya ujenzi wa bustani ya Kijenge kwa kampuni ya Luneco bila kuishirikisha bodi ya zabuni ya halmashauri hiyo.

Katika shtaka la tatu, wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya ambapo Agosti 23 mwaka huu walitoa fedha za serikali sh milioni 45.7 kwa kampuni ya Luneco ambayo haikustahili kwa mujibu wa sheria.
Shtaka la nne, linawakabili washtakiwa wote wanne ambapo inadaiwa kuwa kati ya Septemba 23 na Oktoba 20, 2010 walishindwa kusimamia ujenzi wa bustani ya Kijenge na hivyo kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya sh milioni 25.5.
Washtakiwa wote walikana mashtaka na wako nje kwa dhamana ambapo shauri hilo litarudi mahakamani hapo kwa kutajwa Julai 19, mwaka huu, baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa upelelezi haujakamilika.
Katika hatua nyingine, walimu wa Shule ya Sekondari ya Moshono wameshtakiwa kwa wizi wa zaidi ya sh milioni 11.8 huku mwalimu mkuu wa shule hiyo, Dismas Shewiyo, akidaiwa kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya sh milioni 11.8.

Walimu hao walifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Mwanguga, na kusomewa mashtaka yao na mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Hangi Chang’a kwenye shauri hilo la uhujumu uchumi namba 19/2012.
Shtaka la kwanza linalomkabili mwalimu Desdery Tarimo (38) anayedaiwa kuwa kwa nyakati tofauti kati ya Januari 2008 na Septemba 2009 akiwa mtumishi wa Wizara ya Elimu katika Shule ya Sekondari Moshono aliiba zaidi ya sh milioni 4.8.

Chang’a alidai kuwa mwalimu Nzinyangwa Mcharo, anakabiliwa na shtaka la pili ambapo anadaiwa kuwa kwa nyakati tofauti kati ya Juni 2009 na 2010 akiwa mwajiriwa wa wizara hiyo katika Shule ya Sekondari Moshono aliiba zaidi ya sh milioni 4.6 za shule hiyo.
Aidha shtaka la tatu lilimhusisha mwalimu Leah Makwenda (36), aliyedaiwa kuwa akiwa mwajiriwa wa wizara hiyo katika Shule ya Sekondari ya Moshono aliiba zaidi ya sh milioni 2.3.
Mwendesha mashtaka huyo wa TAKUKURU alisoma shtaka la nne linalomkabili mwalimu mkuu wa shule hiyo, Shewiyo, ambaye anadaiwa katika kipindi cha kati ya Januari 2008 na Septemba 2010 katika ofisi za 

Manispaa ya Arusha, aliisababishia serikali hasara ya zaidi ya sh milioni 11.8.
Washtakiwa wote walikana mashtaka na wako nje kwa dhamana mpaka kesi yao itakapotajwa tena Julai 19 mwaka huu kutokana na upande wa mashtaka kudai kuwa upelelezi haujakamilika.
Katika hatua nyingine Afisa Elimu (vielelezo) wa Manispaa ya Arusha, Godfrey Agustino, alifikishwa mahakamani hapo kujibu mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya sh milioni 11.5 makosa anayodaiwa kuyatenda katika kipindi cha kati ya Julai 2009 na Septemba 2010.
Alisomewa mashtaka hayo na mwendesha mashtaka wa TAKUKURU, Jakopio Richard mbele ya Hakimu Mkazi, Judith Kamara, ambapo shauri hilo limeahirishwa mpaka Julai 17 litakaporudi kwa ajili ya kutajwa.

0 comments:

Post a Comment