0digg
AELEZA MGODI ULIVYOUZWA BEI YA KUTUPA,NGELEJA NAYE AZUA MTAFARUKU BUNGENI Na Ayoub Mangi, Dodoma
SAKATA la ufisadi katika uuzwaji wa mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya limeibuka upya, safari hii ikielezwa na Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono kuwa umeuzwa kwa bei ya kutupa.Mbunge huyo ambaye ni mwanasheria, amelitaka Bunge kuunda Kamati Teule kwenda kuchunguza ufisadi huo, huku akihoji sababu za Serikali kuutengea mabilioni ya shilingi wakati umekwishauzwa.
Mkono alisema kuwa, “Mgodi huo wenye thamani ya matrilioni ya shilingi, umeuzwa kwa bei ya kutupa ya dola 700,000 tu za Marekani (Sh1.1 bilioni), kwa kampuni ya Intra Energy ya Australia.”
Mgodi wa Kiwira uliwahi kuzua malalamiko baada ya kumilikishwa kwa Kampuni ya ANBEN Limited, mali ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na mkewe, Anna Mkapa, lakini Januari mwaka huu, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja aliieleza Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), kuwa ANBEN Limited haihusiki tena na mgodi huo.
Alifafanua kuwa kampuni hiyo iliondolewa kuwa miongoni mwa wamiliki wa hisa kwa vile haikuweza kulipia hisa 200,000 ilizokuwa imechukua wakati wa usajili wa Kampuni ya Tan-Power Resources (TPR).
Akichangia mjadala wa Bajeti jana, Mkono alihoji sababu za Serikali kutenga Sh40 bilioni kwa ajili ya kulipa watu wa mgodi wa Kiwira ilhali inajua kuwa mgodi huo uliuzwa kwa bei ya kutupwa tangu mwaka 2007.
“Tumetenga Sh40 bilioni za kuwalipa watu waliotuibia fedha zetu, eti tunasema kwamba tunalipa madeni, haya ni madeni gani ambayo tunakwenda kulipa huko?” alihoji Mkono.
Alisema mwaka 2007 wabunge walipiga kelele wakiitaka Kampuni ya Tan Power iliyokuwa mbia wa Serikali katika mgodi huo, kuurudisha serikalini, lakini mwaka jana kampuni hiyo iliuza mgodi huo kwa bei ya kutupa.
“Unauzaje mgodi huu wenye thamani ya matrilioni ya pesa kwa bei hii ya kutupa?” alihoji na kuendelea, "Haya ni mambo ya ajabu sana. Tungeweza kupata fedha nyingi sana kutokana na mgodi huu na fedha hizi zingetusadia katika kugharimia mahitaji yetu ya bajeti.”
Mbunge huyo aliungana na wabunge wengine kuiponda Bajeti ya Serikali kwa kutegemea fedha za wahisani, huku rasilimali za nchi zikiendelea kufujwa bila huruma.
Alisema nakisi inayoonekana kwenye Bajeti, inatokana na uwezo mdogo wa kukusanya fedha za ndani licha ya kwamba nchi ina utajiri mkubwa wa madini, ambayo hata hivyo, yanawanufaisha watu wengine na kuwaacha Watanzania wakitaabika.
Mkono pia aliishambulia Serikali kwamba ‘ilichakachua’ mradi wa uchimbaji wa madini katika mgodi wa Buhemba na kuwadanganya wananchi ambao hawakunufaika na kitu chochote.
Kutokana na hilo, mbunge huyo alisema kuwa Bajeti ya mwaka 2012/13 imetoa upendeleo kwa baadhi ya maeneo huku ikiyaacha mengine muhimu, ambayo yanagusa masilahi ya wananchi.
“Serikali ilichakachua Buhemba lakini inapeleka tena Sh1 bilioni huko na sijui zinakwenda kufanya nini wakati ingeweza kupeleka katika moja ya shule za jimboni kwangu, au hata kama ingetusaidia wananchi wa Mara kujenga chuo kikuu cha kilimo ambacho kinajengwa mkoani kwetu,’’alisema Mkono.
Alisema yeye binafsi haelewi Serikali inaposema haina fedha kwani migodi ya Kiwira na Buhemba ingetumika vizuri, ingeweza kuipatia Serikali kiasi kikubwa cha fedha kinacholingana na fedha zinazotolewa na wafadhili.
Ngeleja achafua hewa
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja jana alisababisha mvutano mkubwa ndani ya Bunge na kuondoa utulivu kwa muda, kutokana na mchango wake wa kuiponda Bajeti ya Upinzani.
Ngeleja aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini hadi Mei 4, mwaka huu alipong’olewa na Rais Jakaya Kikwete, aliwabeza wapinzani kuwa Bajeti yao ilikuwa imeandaliwa na watu ambao wana maono ya kuandaa bajeti za harusi na maandamano, lakini si katika hali ya kuandaa Bajeti ya nchi kama Tanzania.
“Mheshimiwa Spika, hawa wenzetu walio mbele yangu hawana jipya, na ningependekeza wasimame na kuwaomba radhi Watanzania maana wameandaa bajeti ya maandamano na harusi,’’ alisema Ngeleja.
Alisema Bajeti ya Upinzani ni ya ovyo na haikuainisha vyanzo mbadala vya mapato na hivyo kuwataka Watanzania kuipuuza.
Huku akishangiliwa na mawaziri na wabunge na CCM, alisema kama viongozi wa upinzani wanaitakia mema Tanzania, ni vyema wakatumia nafasi zao ndani ya Bunge kusimama na kuwaomba radhi wananchi kwa kuwa wamesababisha baadhi kutoijali mipango mizuri ya Serikali.
Hali hiyo ilisababisha wabunge wengi wa Chadema kusimama na kuomba Mwongozo wa Spika kuhusu jambo hilo.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee walipewa nafasi ya kuzungumza, huku Ngeleja akipinga kila kitu walichosema.
Mdee alimweleza Spika kuwa tatizo la Ngeleja siyo kupingana na maoni ya Kambi ya Upinzani bali ni hasira za kuondolewa katika nafasi ya uwaziri wa Nishati na Madini, jambo ambalo bado linamuuma.
“Mheshimiwa Spika, hakuna kitu kama hicho, tatizo la Ngeleja ni kuondolewa katika nafasi ya uwaziri na siyo kitu kingine, maana kama ni maneno ambayo yalikuwa yamekosewa tayari tulishaleta mabadiliko yake humu ndani,” alisema Mdee, kisha akakubaliana na Spika, kuondoa maneno kuwa tatizo la Ngeleja ni uwaziri.
Kwa upande wake Mbowe, alisema kuwa Ngeleja hakusoma bajeti yao vizuri na kumwomba Spika kutoa tamko la namna ya kuwashughulikia wote wanaodanganya umma katika michango yao.
Lissu alitoa ufafanuzi ulioafikiwa na Spika, kuwa Bajeti inayojadiliwa bungeni ni moja ambayo ni ya Serikali, na kwamba Kambi ya Upinzani haina ya kwake, bali inatoa maoni kwa ile ya Serikali.
0 comments:
Post a Comment