Mabaunsa waunda umoja
Watu
wanaodaiwa kuwa ni "mabaunsa" wameunda umoja wao na kuanza kukusanya
ushuru kutoka kwa Wamachinga wanaopanga bidhaa zao katika kituo cha
daladala cha Mwenge Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mabaunsa hao wamedaiwa kufanya zoezi hilo
huku wakishirikiana na baadhi ya watendaji wa Manispaa ya Kinondoni
ambao wanawapa sehemu ya mapato wanayoyapata kutoka kwa wafanyabiashara
hao.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini
kuwa "mabaunsa" hao ni sehemu ya wafanyakazi wa iliyokuwa kampuni
iliyopewa tenda ya kukusanya ushuru wa daladala katika kituo hicho
ambayo hata hivyo inadaiwa imemaliza muda wake wa kufanya kazi hiyo.
Watu hao wanadaiwa kukusanya kati ya Sh.
500,000 hadi 1,000,000 kutegemea wingi wa wafanyabishara kwa siku hiyo
ambao wanapanga bidhaa zao kwenye meza na wengine wanaozishika mikononi
kuanzia asubuhi hadi usiku.
Baadhi ya wafanyabishara hao ambao
wanaendesha bishara zao kituoni hapo, waliliambia NIPASHE kuwa meza moja
inalipiwa kati ya Sh. 5,000 hadi Sh. 7,000 kutegemea na ukubwa wa meza
na kwamba fedha hizo zinatolewa kila siku.
Katika kituo hicho kuna zaidi ya meza 100
zilizozunguka eneo zima huku idadi ya wamachinga wanaotozwa ushuru bila
ya kuwa na meza ikiwa haijulikani lakini fedha hizo zinadaiwa
kuchukuliwa na mabaunsa bila kutoa stakabadhi.
Wamesema mtu anayekataa kulipa ushuru huo,
anapigwa na watu ambao walidai wana miili mikubwa pamoja na
kuwanyang'anya bidhaa zao zilizopo mezani na kwa wale wanaokuwa
wamezishika mikononi.
Hata hivyo, walisema licha ya kulipa kiasi
hicho cha fedha hawapewi stakabadhi na kwamba mfanyabiashara
anayejaribu kudai anapigwa na kupelekwa kituo kidogo cha Polisi Mwenge.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa serikali ya
mtaa wa Mwenge, Pascal Ng'itu alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kusema
kuwa watu hao wamekuwa wakifanya kazi hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja hadi
sasa.
Alisema wafanyabiashara hao licha ya kuwa
wapo katika eneo hilo kinyume cha sheria lakini kimeibuka kikundi cha
watu wanaowalipisha ushuru huku mapato hayo yakiwa hayajulikani
yanapelekwa wapi.
Alifafanua kuwa kwa muda wa mwaka mmoja,
hakuna Mkandarasi anayejulikana kisheria ambaye amepewa kazi ya
kukusanya mapato yatokanayo na ushuru wa magari ya daladala yanayotumia
kituo hicho.
Ng'itu alisema kwamba kampuni iliyoshinda
tenda ya kukusanya mapato katika kituo hicho, imenyimwa kazi hiyo na
badala yake watu wasiojulikana ndiyo wanaoendelea kukusanya fedha
zinazolipwa na daladala.
"Hiki kituo mimi kama mwenyekiti naona
kuna uchafu mwingi na wa kutisha kwa sababu watu wanaokusanya ushuru
haijulikani wanazipeleka wapi na ni kiasi gani kinachopatikana," alisema
Kwa mujibu wa taratibu za Manispaa ya
Kinondoni, kampuni inayopewa tenda ya kukusanya ushuru inatakiwa
kusimamia mapato yatokanayo na daladala, kuwaondoa wafanyabiashara ndogo
ndogo, kukiweka kituo katika hali ya usafi pamoja na kuwaondoa wapiga
debe.
Mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya
Kinondoni, Fortunatus Fwema alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema
ameshtushwa huku akisema kwamba hajui kama kuna kikundi cha watu
kinakusanya ushuru kutoka kwa wamachinga.
Alisema wamachinga hao wapo kituoni hapo
kinyume cha utaratibu, lakini akasema pia watu wanawatoza ushuru
wanahesabiwa kama wahalifu na kwamba watasakwa na Manispaa.
Alisema juhudi za kuwaondoa wamachinga
pamoja na kumpata mkandarasi wa kukusanya ushuru zinafanyika na kwamba
siku yoyote kuanzia sasa watavamia kituo hicho ili kuwatoa.
Alisema baada ya kumaliza kazi ya
kuwaondoa wamachinga katika eneo la Ubungo na Tegeta kwa sasa zoezi hilo
litahamia Mwenge muda wowote ili kuhakikisha kituo kinabaki wazi kwa
ajili ya kuhudumia daladala.
Aliahidi kufanya uchunguzi wa kina ili
kubaini watendaji wa Manispaa wanaoshirikiana na kikundi hicho kukusanya
ushuru kinyume cha sheria wala kufuata taratibu.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment