Friday, June 29, 2012

Picture
Mwenyekiti wa Bodi, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Norman Sigara akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu kusimamishwa kazi kwa Madaktari hao
Bodi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, imewasimamisha kazi madaktari 72 kwa kosa la kutoingia kazini kwa siku tano jambo ambalo ni kinyume cha makubaliano ya mkataba.

Madaktari hao ni 54 wa mafunzo ambao waliingia mkataba wa miaka miwili na hospitali ya Rufaa na Madaktari 18 walioajiriwa na Wizara ya afya.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Bodi, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Norman Sigara, alisema kitendo cha madaktari kutoripoti kazini kwa siku tano ni ukiukwaji wa kanuni za utumisha wa umma toleo la 2009 kifungu namba F.16-F17 na F. 27.

"Hivyo kupitia kanuni hiyo madaktari hao wamesimamishwa kazi na kurudishwa kwa mwajiri wao ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa hatua zaidi za kinidhamu,"alisema Sigara.

Imeelezwa kuwa, siku ya tarehe 23/6/2012 wafanyakazi 15 waliokuwa zamu (Intern Doctors 12 na Registrars3) hawakufika kazini na tarehe 24/6/2012 wafanyakazi 19 (Intern doctors 15 na Registrars 4) hawakufika kazini.

Alisema, kuanzia tarehe 25/6/2012 imethibitika kuwa Interns Doctor 54 na Registrars 18 hawakufika kazini hadi leo tarehe 28/6/2012. Tarehe 25/6/2012, bodi ya hospitali ilifanya kikao cha dharura kujadili hali ya utendaji kazi na utoaji huduma hospitalini na kutoa uamuzi.

Sigara, aliyataja maamuzi hayo kuwa ni Mwenyekiti wa Bodi akutane na madaktari ambao hawakufika kazini ili awasikilize sababu za kutofika na kujadili namna ya kumaliza matatizo hayo jambo ambalo madaktari hao waligoma.

Alisema, baada ya madaktari hao kukaidi ombi hilo, Bodi ya hospitali iliwaandikia barua za kujieleza kwanini wasichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuvunja mkataba walioingia na hospitali na pia kukiuka kanuni za kudumu za utumishi wa umma nalo walilikaidi.

"Iwapo madaktari ambao hawakuripoti au kueleza sababu za kuridhisha ifikapo tarehe 28/6/2012. kwa kuzingatia kanuni za utumishi wa Umma, madaktari hao watasimamishwa kazi na kurudishwa kwa mwajiri wao ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii," alisema.

Aidha, alisema kuwa kwa ujumla madaktari hao waligomea barua zote mbili, yaani ya kuitwa kwenye kikao pamoja na ile ya kuwataka kujieleza hivyo Bodi imechukua hatua za kisheria za kuwafukuza kazi.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti huyo wa bodi alisema kuwa tayari hospitali ya Rufaa kwa ushirikiano wa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, madaktari watano wamepatikana ili kusaidia huduma kwa hospitali hiyo.
                                                      Via Mbeya yetu blog

0 comments:

Post a Comment