• Makanisa, magari yachomwa moto
MACHAFUKO makubwa yameukumba mji wa Zanzibar juzi na jana,
ambapo kanisa moja limelipuliwa na kitu kinachoaminika kuwa bomu la
kurusha kwa mkono, huku kukiwa na madai kuwa Watanzania wenye asili ya
Bara wanaoishi na kufanya kazi visiwani hapa wameshambuliwa.
Mashuhuda wameliambia Tanzania Daima kwamba, watu ambao hadi sasa
hawajajulikana, lakini wakiaminika kuwa ni wafuasi wa kundi la kidini la
uamsho, walilishambulia na kulilipua Kanisa la Tanzania Assemblies of
God la Kariakoo, visiwani hapa kuharibu magari, miundombinu na mali
nyingine.
Taarifa hizo zilizothibitishwa na Jeshi la Polisi, zimesema kuwa,
wafuasi wa kundi hilo walianza vurugu hizo juzi, wakipinga kitendo cha
kukamatwa kwa kiongozi wao, Mussa Juma kwa kosa la kufanya maandamano
bila kibali cha polisi.
Habari zimedai kuwa, baada ya kukamatwa kwa kiongozi huyo, wafuasi
wake walianza kuhamasishana kwenda Kituo cha Polisi Madema, kilichoko
Wilaya ya Mjini Magharibi wakiwa na silaha za mawe, jambo lililowafanya
polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.
Hata hivyo, habari zinadai kuwa, baada ya kutawanyika, majira ya saa
mbili usiku wafuasi hao walianza kuziba barabara kwa mawe na magogo
makubwa, kuchoma matairi katika maeneo ya Michenzani, kabla ya
kuyashambulia na kuyaharibu vibaya magari kadhaa.
Aidha, mashuhuda wamedai kuwa, baadhi ya wafuasi hao walianza kuzisaka
nyumba za ibada na ndipo walipokwenda lilipo kanisa hilo, na kuanza
kulishambulia kwa mawe, kabla ya kulilipua kwa kitu kinachoaminika kuwa
bomu.
Kadhalika, kuna madai kuwa wafuasi wengine wa kundi hilo, walijigawa
na kuanza kuzifuatilia nyumba wanamoishi wafanyabiashara na wafanyakazi
wanaotoka Tanzania Bara na kuzishambuli kwa mawe, huku wakitoa maneno ya
vitisho.
Mmoja wa wafanyakazi hao kutoka Bara, anayefanya kazi katika hoteli
moja ya kitalii (jina linahifadhiwa), alikiri nyumba yao kushambuliwa
vikali, na jana alilazimika kuhamia kwa rafiki zake ambao ni wenyeji wa
visiwani hapa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Musa Ali katika
taarifa yake jana kwa vyombo vya habari, amekiri kuharibiwa kwa kanisa
hilo, na kwamba hadi jana mchana watu saba walikuwa wakishikiliwa na
jeshi hilo.
Kamishina Ali alisema, kundi hilo katika mwendelezo wake wa kufanya
mikusanyiko kwa ajili ya makongamano, mihadhara, dua na itkafu, juzi
lilikuwa katika viwanja vya Lumumba majira vya asubuhi kwa dhamira ya
kusasababisha watu wauchukie Muungano na kuitaka serikali iitishe kura
ya maoni kuhusu kuendelea, au kutoendelea kwa Muungano na serikali zake.
Alisema pamoja na kufanya matendo mengine ya uvunjifu wa amani kinyume
na lengo la kuanzishwa kwa jumuia hiyo na katiba yao, majira ya saa za
mchana viongozi wao waliwahamasisha watu waliokuwa katika kongamanao
hilo kufanya maandamano bila kuarifu polisi.
Kamishna Ali alidai, kutokana na historia ya nyuma ya kundi hilo,
polisi walilazimika kuyavunja kwa vile katika siku za karibuni jumuiya
hiyo ilikwishaonesha dalili za uvunjifu wa amani kwa kufanya matendo
mbalimbali, ikiwemo kutoa lugha ya matusi kwa viongozi wa serikali na
wananchi ambao hawakuwaunga mkono.
Alisema kundi hilo limekuwa likifunga barabara bila sababu, kutembea
na ving’ora isivyo halali, kuwashambulia watu kwa silaha zenye ncha
kali, kuharibu mali za watu kama magari, na vingine vya aina hiyo.
Kutokana na tukio hilo, polisi wametangaza msako mkali wa viongozi na
wanaokifadhili kikundi hicho kwa gharama yoyote, na waliohusika na
vurugu hizo na kwamba watakaopatikana watafikishwa mahakamani kujibu
mashitaka.
Kamishna huyo amesema polisi na vikosi vya usalama wameimarisha ulinzi
kuhakikisha kuwa usalama wa maisha ya watu na mali zao unadumishwa kwa
gharama yoyote.
CHADEMA wailaumu serikali
Jijini Dar es Salaam, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kimesema Rais Jakaya Kikwete, Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na
CCM wamesababisha mivutano na vurugu Zanzibar kwa kutaka kudhibiti
mjadala kuhusu muundo wa muungano na uhuru wa nchi katika mchakato wa
katiba mpya kwenye suala hilo tete na tata.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Habari wa Uenezi wa chama
hicho, John Mnyika ambaye alisema mivutano na vurugu zinazoendelea
Zanzibar ni matokeo ya Serikali ya Muungano na ya Mapinduzi Zanzibar
kutokuzingatia mapendekezo ya chama hicho kuhusu umuhimu wa uhuru wa
mjadala kuhusu muundo wa muungamo katika mchakato wa katiba mpya.
Aidha, alisema mvutano huo umeshika kasi baada ya maamuzi ya NEC ya
CCM bila ya maoni ya wanachama wake wa Zanzibar na Tanzania Bara kuminya
mjadala kuhusu suala hilo.
CHANZO CHA HABARI. gazeti la Tanzania Daima http://www.freemedia.co.tz/daima/
0 comments:
Post a Comment