Kocha msaidizi wa timu ya Yanga, Fred Felix Minziro
Wazee hao waliwaambia wanahabari jijini Dar es Salaam jana kuwa wana pesa Sh. milioni 750 kwa ajili ya kuiokoa na kuiendesha klabu hiyo ambapo watalipa mishahara wanayodai wachezaji, wafanyakazi wote wa klabu hiyo, akiwemo kocha msaidizi Fred Felix Minziro na wengineo.
Katibu wa baraza hilo, Ibrahim Akilimali, alisema kuwa hawautambui mkutano mkuu wa Yanga uliotangazwa na Nchunga kwamba utafanyika Julai 15, lakini watakuwa tayari kuugharamia kuanzia kukodi ukumbi, chakula na kila kitu endapo atakuwa ameshajiuzulu kabla ya muda huo.
Alipoulizwa endapo uongozi wa Nchunga utazuia kufanyika kwa mkutano wao wa Jumapili klabuni hapo, Akilimali atakuwa amechochea "mvua ya masika ambayo itanyesha Jangwani."
"Mkutano wetu tutaufanyia klabuni hata kama atazuia," alisema Akilimali.
Akizungumzia suala la Nchunga kutafuta kocha kwa ajili ya kuinoa klabu hiyo, alisema endapo atajiuzulu na kuacha jina la kocha ambaye alianza harakati za kumtafuta, wao watakaa chini kulijadili na kama wataona linafaa wataendeleza kile alichoacha.
"Akijiuzulu tupo tayari kuendeleza mazuri atakayoyaacha," alisema Akilimali.
Akizungumzia suala la kocha Kostadin Papic aliyetangaza kurejea endapo mwenyekiti huyo atajiuzulu, Akilimali alisema hawezi kulizunguzia suala hilo. "Papic atabakia kuzungumza yeye kama Papic," alisema.
Akilimali alisema wajumbe wa kamati iliyo chini ya Nchunga, watakaowahi kujiuzulu nyadhifa zao, baraza la wazee litaendelea kuwahudumia hadi mikataba yao itakapomalizika, huku akisisitiza kwamba kwa watakaong'ang'ania madarakani hadi watakapong'olewa kwa nguvu, watapoteza haki zao.
Kufuatia madai kwamba wazee wanatumiwa na watu fulani wenye pesa ili kuivuruga timu hiyo, Akilimali alisema si kweli na kwamba fedha hizo zipo katika akaunti zao.
Akilimali aliwaponda wanaodai kuwa wazee hao wanaitaka timu wakati hawana pesa huku wakiwa wanaishi katika nyumba za kupanga, ambapo alihoji kwani wakichua timu, wachezaji wataenda kuishi nao makwao? Na akatamba kwamba yeye anazo nyumba saba.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment