Takriban mwezi mmoja sasa toka kufariki
kwa msanii maarufu nchini, Steven Kanumba, huku msanii mwenzake
Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu akiwa anaendelea kushikiliwa
na vyombo vya dola kwa ajili ya uchunguzi kuhusiana na kifo hicho,
vyombo vya habari vimeendelea kulivalia njuga suala hilo huku habari
nyingi zikiwa zimejikita kwa mtuhumiwa Lulu.
Mengi yanazungumzwa kuhusu msanii huyo,
kama ambavyo pichani vichwa vya habari vya baadhi ya magazeti
vinajieleza. Hali hii kwa kiasi kikubwa imekuwa ikikinzana na taratibu
za kisheria juu ya kuandika habari zenye kumhusu mtuhumiwa wa kosa
fulani.
Bila kujali kilichomo au alichomaanisha
mwandishi, ni wazi kuwa kwa ujumla wake, habari hizi zina athari ya
namna yake kwa jamii inayosoma habari hizo na yenye kumfahamu Lulu, huku
jamii hiyo ikiwa na hisia mchanganyiko kuhusu binti huyo.
Jambo lililo wazi ni kuwa, kwa kiasi
fulani ni habari ambazo zimekuwa zikitengeneza picha fulani miongoni mwa
jamii, picha ambayo kwa namna moja ama nyingine, kwa njia hasi au
chanya, zinaweza kuathiri uchunguzi wa tukio hilo hali ambayo itakuwa na
athari kubwa sana kwa upande wa Jamhuri unaoendesha uchunguzi wa suala
hilo na Lulu mwenyewe kwa upande mwingine.
Ni katika mazingira haya basi, ambapo
nimekuwa nikijiuliza kuwa, Je, tunamtendea haki Lulu kupitia maandishi
yetu? Je, tunautendea haki upande unaofanya uchunguzi wa suala hili? Au
maslahi yetu ya kibiashara ndio pekee tunayoyajali bila kuangalia upande
wa pili?
0 comments:
Post a Comment