Saturday, May 19, 2012

MAOMBI ya uchunguzi wa umri wa muigizaji wa filamu, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu anayekabiliwa na  kesi ya mauaji, yamepangwa kusikilizwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam  Mei 28, 2012.

Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.Hata hivyo, umri wake halali umezua utata kiasijambo ambalo limewalazimu Mawakili wanaomtetea kuwasilisha maombi mahakamani wakiitaka mahakama ifanye uchunguzi wa umri halali wa msanii huyo.

Maombi hayo yaliwasilishwa Mahakama Kuu na mmoja wa mawakili wake, Peter Kibatala, Mei 17.

Habari ambazo Mwananchi lilizipata jana kutoka mahakamani hapo na kuthibitishwa na Wakili Kibatala zinasema kuwa maombi hayo yamepangwa kuanza kusikilizwa Mei 28 na kwamba yamengiwa kusikilizwa na Jaji wa Dk Fauz Twaib.

Katika maombi namba 46 ya mwaka 2012, mawakili hao wanaomtetea msanii huyo wanaiomba Mahakama Kuu itoe uamuzi kama Mahakama ya Kisutu ina uwezo wa kuamua ufanyike uchunguzi wa umri halali wa msanii huyo.
Jopo la mawakili hao maarufu linadai kuwa linaamini kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambayo kwa sasa ndio bado inayoshughulikia kesi hiyo, ina mamlaka ya kufanya au kuamuru ufanyike uchunguzi wa umri mshtakiwa huyo.

Lakini pia wanaiomba Mahakama Kuu kama itaridhika kuwa Mahakama ya Kisutu haina uwezo huo, basi Mahakama Kuu yenyewe ifanye uchunguzi huo.

Mawakili hao walifikia uamuzi wa kuwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu baada ya maombi ya Mahakama ya Kisutu kujiondoa katika kuyashughulikia.

Akifafanua juu ya maombi hayo Kibatala ambaye pia ni Makamu wa Raisi wa Chama cha Wanasheria nchini (TLS) alisema kuwa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 kifungu cha 113 inaruhusu Mahakama kufanya uchunguzi wa umri wa mshtakiwa.

Wakili Kibatala alisema lengo la uchunguzi huo ni  ili mahakama iweze kujiridhisha kama mshtakiwa ni mtoto au ni mtu mzima kwa lengo la kujipa angalizo juu ya maslahi ya mtoto.

“Baada ya uchunguzi huo mahakama ikijiridhisha kuwa ni mtoto basi mwenendo wa kesi hiyo utaendeshwa kwa maslahi ya mtoto kwa mujibu wa kifungu cha 4(2) cha sheria hiyo ya mtoto,” alisema Wakili Kibatala.

Kwa mujibu wa Wakili Kibatala kifungu hich ambacho huelezea ulinzi wa maslahin ya mtoto katika uendeshaji wa kesi kwa watoto wanaokinzana na sheria.
Kabla ya kuwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu, mawakili hao mawakili hao waliwasilisha maombi  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mei 7,2012  wakiiomba iamuru kesi ya msanii huyo isikilizwe katika mahakama za watoto wakidai kuwa bado ni mtoto.

Mawakili hao walidai mahakamani hapo kuwa msanii huyo ana umri wa miaka 17 na kwamba kwa maana hiyo yeye bado ni mtoto na kesi yake haipaswi kusikilizwa katika mahakama za kawaida kama mtu mzima.
Kiongozi wa jopo la mawakili wanaomtetea msanii huyo wakili Kenedy Fungamtama alidai kuwa mteja wao ana umri wa miaka 17 na si 18 kama inavyotamkwa mahakamani.

Alidai kuwa hata cheti cha kuzaliwa walichokiwasilisha mahakamani kinaonyesha mahali na tarehe aliyozaliwa mshtakiwa hivyo kuwa na umri wa miaka 17.

“Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inatafsiri kuwa mtoto ni yule aliyekuwa na umri chini ya miaka 18 hivyo katika suala la mteja wetu alipaswa kushtakiwa katika mahakama ya watoto,” alidai Wakili Fungamtama.

Hata hivyo upande wa mashitaka kupitia kwa wakili Elizabeth Kaganda ulipinga maombi hayo na kudai kuwa bado wanaendelea na upelelezi wa kesi hiyo na hivyo kuomba wapewe muda zaidi.
Wakili Kaganda pia alidai kuwa hata jina linaloonekana katika cheti cha kuzaliwa cha mshtakiwa huyo linasomeka kama Diana Elizabeth wakati mshtakiwa huyo ametajwa mahakamani hapo kama Elizabeth Michael.

Akijibu hoja hiyo, wakili Fungamtama alikiri jina hilo kusomeka Diana Elizabeth na kusema kuwa ni jambo la kawaida hasa kwa wakristo kuwa na majina mawili

Katika uamuzi wake, Mkazi Augustina Mmbando anayesikiliza kesi hiyo alisema kesi hiyo bado iko kwenye upelelezi na kwamba kulingana na jinsi ilivyo isingekuwa busara kuamua hoja yoyote.
Hivyo Hakimu Mkazi Augustina Mmbando anayesikiliza kesi hiyo, aliutaka upande wa utetezi uwasilishe maombi hayo kupitia Mahakama Kuu.

Mbali na Kibatala na Fungamtama ambaye pia anaitetea Kampuni ya kufua umeme wa dharua ya Dowans dhidi ya Tanesco, mawakili wengine katika jopo hilo ni Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) Joaquine De- Melo.

De-Melo ambaye amewahikuwa Rais TLS, pia ni mshindi wa  wa tuzo ya Mwanamke Jasiri Tanzania ya Martin Luther King. Jopo la mawakili hao wanaomtetea msanii huyo linahitimishwa na Fulgence Massawe kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)

Msanii huyo bado anaendelea kusota rumande kutokana na kesi inayomkabili kutokuwa na dhamana na kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Mei 21 mwaka huu.

0 comments:

Post a Comment