Waziri Mkuu wa Kenya Raila
Odinga amejibu hatua ya naibu wake Musalia Mudavadi kukihama chama cha
Orange Democratic Movement (ODM) na kusema alikuwa huru kuchukua uamuzi
wake.
Akizungumza na BBC mjini London, Odinga amesema
kama kiongozi anayetetea demokrasia, hawezi kushtumu uamuzi wa naibu
wake ambaye amejiuzulu pia kama waziri wa serikali za mitaa.
Aidha
Odinga ambaye ni kiongozi mkuu wa chama cha ODM amesema ataachia baraza
kuu la chama kuamua ikiwa itamuondoa kwenye chama Mudavadi na hivyo
kupoteza kiti chake cha ubunge hatua ambayo huenda ikamfanya Naibu
Waziri Mkuu kurudi kwenye uchaguzi katika jimbo lake la Sabatia,
Magharibi mwa Kenya.
Kuhusu ikiwa ODM itayumba kisiasa kufuatia
kuondoka kwa Mudavadi, Odinga amesema chama hicho kina wafuasi wengi na
kujiondoa kwa Mudavadi hakuna athari zozote.
Tofauti kati ya Musalia Mudavadi na Raila Odinga
zilichochewa na kanuni za uteuzi wa mgombea wa Urais wa ODM ambapo
wanaomuunga mkono Mudavadi ulilalamika kuwa washirika wa Waziri Mkuu
walipenyeza vipengele vinavyomzuia Naibu Waziri Mkuu kuwania urais kwa
tiketi ya chama hicho.
ODM imekumbwa na mpasuko mkubwa miongoni mwa
wanasiasa wake ambapo tayari aliyekua naibu kiongozi wa chama hicho
William Ruto alikihama chama na kufuatwa na wabunge waliomuunga mkono.
Nchini Kenya wabunge wamekuwa wakihama hama
vyama ambavyo viliwafadhili kuingia bungeni bila kuwasilisha waraka wa
kuachia ubunge kama inavyotakiwa kisheria.
0 comments:
Post a Comment