Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM Nape Nnauye
---
Hivi karibuni chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
kilielezea kile ilichoeleza kuwa ni kutishwa na wimbi la mauaji
yanayotishia amani ya nchi kikidai kuwa jumla ya wanachama wake 15
wameuawa katika wilaya ya Igunga peke yake.
Madai hayo ya CHADEMA, pamoja na wanachama wengine na
mashabiki wao, yalitolewa na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe,
ambaye alidai kuwa mauaji hayo yana mkono wa serikali ya CCM, ambayo kwa
madai yao imeona wazi kuwa upepo wa kisiasa umekiendea vibaya na sasa
kinataka kujiimarisha katika utawala kwa kuua watu wanaoipinga.
Akifungua kikao cha Baraza Kuu la chama hicho jijini
Dar es Salaam Aprili 29 mwaku huu mwenyekiti huyo alifafanua kuwa mbali
na kuuawa kwa watu wanne kwa pamoja na juzi kifo cha mwenyekiti wao wa
tawi huko Arumeru mkoani Arusha, jumla ya wanachama wake 15 wameuawa
katika wilaya ya Igunga peke yake tangu kumalizika kwa uchaguzi mdogo wa
jimbo hilo mwaka jana.
Mbowe katika maelezo yake alijaribu katika maeneo
kadhaa kuihusisha CCM na au serikali yake katika matukio kadhaa
yaliyowakabili baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema katika maeneo
mbalimbali nchini likiwemo lile la Mbunge Highness Kiwia ambaye Suala
lake bado Lipo mikononi mwa vyombo Vya dola likishughulikiwa.
Katika sehemu kubwa ya maelezo ya Ndg. Mbowe
amejitahidi kuonesha kuwa mauaji yote yaliyoikabili na yatakayokuwa
yakiikabili Chadema kupitia wafuasi wake yanafanyika kisiasa, Jambo
ambalo ni la uzushi, kwani Halina ushahidi wa kisheria hata kimazingira,
wa Moja kwa Moja unaoondosha ujinai au makosa hayo, na kuwa ni makosa
yanayolenga muktadha wa kisiasa.
Huku akitaka kuuaminisha umma kuwa huo ndio ukweli,
Ndg. Mbowe amesisitiza kuwa hilo lime kuwa likitekelezwa na CCM kwa
lengo la kuwatisha wananchi kujiunga na chama hicho hoja ambayo haina
msingi wowote wa kiutafiti.
Hivyo CCM kwa kutambua kuwa Suala la mauaji linabeba
Kosa la jinai, na kwa kuwa Ndg. Mbowe ameshutumu Moja kwa Moja CCM na
serikali yake kuihusisha na mauaji hayo, ni vema sasa nasi tukatoa
msimamo wetu dhidi ya tuhuma, hiyo.
Kwanza, si busara hata kidogo kuihusisha CCM katika
matukio hayo, kwani uchunguzi unaofanywa na vyombo vya dola umeshindwa
mpaka sasa kuhusisha matukio hayo na siasa, badala ya kuyahusisha na
makosa ya jinai ambayo hufanywa na watu kwa malengo tofauti na yale
ambayo Ndg. Mbowe anataka kuwaaminisha watu.
Pili, CCM haijawai, haiwezi, na haitakuja fanya jambo
lolote lenye lengo la kuvuruga Amani na Usalama wenye utulivu ndani ya
taifa letu, hivyo uzushi na usingiziaji uliofanywa na Mtu Kama Ndg.
Mbowe, si vema kuuacha kimya, badala yake nimetumia wasaa Huu muhimu
Kujibu, na kutoa ufafanuzi ili Kuupa umma wa watanzania habari sahihi.
Ni aibu kwa Chama kama Chadema kujitahidi kwa nguvu
zote kujaribu kuficha ukweli wa mauaji yanayotoa roho za watanzania
wenzetu kwa kuyapa sura ya kisiasa. Hizi ni juhudi za makusudi za kutaka
kuficha ukweli wa kinachotokea.
Ni aibu kwa chama kama Chadema kujaribu kutumia mauaji
mabaya kama haya kutafuta mtaji wa kisiasa. Huku ni kuonyesha jinsi gani
wamefilisika kisiasa mpaka wanafikia mahali pa kuamini kuwa wanaweza
kutumia chochote kama mtaji wa kisiasa, vikiwemo vifo vya watanzania
wenzetu. Huku si kufilisika tu ila kwakweli ni unyama unaotakiwa
kulaaniwa na kila muungwana.
Imetolewa na:
Nape Moses Nnauye
Chama Cha Mapinduzi
Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi CCM
0 comments:
Post a Comment