Saturday, May 12, 2012

“SERIKALI ingekuwa inaamini ushirikina, ningemrudisha mwanangu Kanumba, maana najua hajafa, bali amechukuliwa msukule…” hivyo ndivyo alivyoanza kuzungumza Flora Mtegoa au Mama Kanumba ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita aliamua kutoboa siri nzito ya moyoni mwake, Ijumaa Wikienda limeshiba data.
Mama Kanumba aliyaongea hayo nyumbani kwa marehemu, maeneo ya Vatican City Hotel, Sinza jijini Dar es Salaam.
Hii ni mara ya kwanza kwa mama huyo kufunguka kwa undani ikiwa ni siku 23 tangu afariki mwanaye Kanumba na kuzikwa kwenye makaburi ya Kinondoni, Dar.

MSUKUMO WA KUTOBOA SIRI
Mama Kanumba akiwa nyumbani hapo na mwandishi wetu, alimpigia simu mwanaume mmoja aliyemtaja kwa jina la Ayubu akidai ni ndugu wa marehemu kwa upande wa baba mzazi, Mzee Charles Kusekwa.
Kwa wakati huo, Ayubu alikuwa Shinyanga akamuunganisha na mwandishi wetu.

KISA CHAANZA KWENYE MALI ZA MAREHEMU
Akianika kila kitu kwenye simu, Ayubu alianza kwa kudai Baba Kanumba ni kigeugeu kwa familia huku akijua mila za Kisukuma haziendani na matakwa yake.
“Unajua ndugu mwandishi namshangaa anko (Baba Kanumba), anawezaje kugombea mali za marehemu wakati hakumtolea mahari Mama Kanumba? Hii mila amejitungia mwenyewe, Kisukuma hatakiwi  kuuliza mali maana hakumtolea mahari mama wa marehemu,” alisema Ayubu.

YALIYOIBUKA KATIKA MAZUNGUMZO
Katika mwendelezo wa mazungumzo hayo, ndipo mazito nyuma ya pazia yakaibuka kwani Mama Kanumba aliweka wazi kuwa kwa sasa mali za marehemu zinamfanya atishiwe maisha na Baba Kanumba.
Aidha, mama huyo wa marehemu alifika mahali akasema kuwa amekuwa akipokea simu za vitisho ambazo zinamtaka akumbuke alipo mwanaye, hivyo akifanya mchezo na yeye atamfuata huko lakini kisa kikubwa kikitajwa kuwa ni mali za marehemu Kanumba.
Mama Kanumba akatoa wito: “Watanzania niombeeni sana, maana natishiwa maisha sasa, naulizwa kama najua alipo mwanangu, nikifanya mchezo na  mimi nitakwenda huko.”
Ijumaa Wikienda lilimwelekeza mama huyo kwamba kama anahisi anaishi kwa wasiwasi kufuatia vitisho hivyo ni bora akafungua kesi ili kujiweka salama zaidi. Lakini mpaka tunakwenda mtamboni hatukufanikiwa kupata RB ya kesi hiyo.

KANUMBA ALIONYWA JUU YA KIFO CHAKE
Akizidi kuweka wazi siri nzito, mama huyo wa marehemu alisema mwanaye alijulishwa juu ya kifo chake.
Alisema mtu aliyedaiwa kumpa tahadhari hiyo ni ndugu wa karibu wa Kanumba (jina halikutajwa) akiambiwa kuwa kuna mganga wa kienyeji Shinyanga (jina linahifadhiwa) anatumiwa kuuondoa uhai wake.
Hata hivyo, alisema marehemu alikuwa akidharau kwa vile hakuwa akiamini ushirikina ingawa siku zilivyozidi kukatika, aliamua kuita watumishi wa Mungu na kufanya misa nyumbani kwake, Sinza.
“Kanumba alionywa na ndugu yake mmoja, akamwambia huku Shinyanga si kwema kwako, kuna tetesi kwamba yupo mtu anakuwinda kukutoa roho. Hakikisha unasali sana Mungu akusaidie,” alisema mama Kanumba akimkariri ndugu huyo.
Akaendelea: “Alipuuzia kwa sababu hakuwa mshirikina, lakini kuna siku alifanya misa nyumbani kwake ili Mungu amsaidie kumlinda na shetani huyo na siku chache mbele ndiyo akafariki dunia.”

MGANGA ALIVYOFANYA KAZI
Katika kile kinachodaiwa kuwa Kanumba amechukuliwa msukule, tamko linalotoka kwa mama na kaka wa marehemu ni kwamba mganga mmoja mashuhuri mjini Shinyanga anadaiwa kufika katika eneo lililotengwa kwa ajili ya kufanya kafara ya kumwondoa Kanumba.
“Unajua tuliambiwa kuwa huyo mtu aliyekuwa akiisaka roho ya marehemu alimwita mganga huyo ambaye alifika nyumbani wiki tatu kabla ya kifo cha Kanumba  na kufanya makafara yaliyokuwa na damu na jina la Kanumba.
“Aliyetuambia mchezo mzima alidai kuwa katika kufanya kafara hilo, mganga alichukua damu na kuchora jina la Kanumba huku akisema kuwa haitachukua siku, ataaga dunia,” alisema Mama Kanumba.

MAMA AAMBIWA MWANAYE HAJAFA, WAENDA KWA NABII MWINGIRA
Mama Kanumba aliendelea kuweka wazi kwamba kifo cha mwanaye kilitokea yeye akiwa Bukoba, alipotua Dar kabla ya mazishi, kuna mtu alimpasha habari za kutisha kuwa Kanumba hajafa, kachukuliwa msukule.
Akasema: “Ilibidi Jumatatu (Aprili 9, 2012) tutume wanandugu kwenda Kanisa la Efatha kwa Mchungaji na Nabii Josephat Mwingira kwa ajili ya maombi ya kumrudisha marehemu baada ya kuambiwa alichukuliwa msukule.”
“Mwanangu (mwandishi) ulishawahi kusikia misukule inarudi? Ndicho kilichotokea, hakurudi hata baada ya maombi yale.”

KISA CHA MWILI WAKE KUTOAGWA NA UMATI LEADERS CHABAINIKA
Siri ziliendelea kuvuja, mwanafamilia mmoja naye akasema kuwa pamoja na umati kujitokeza kwenye Viwanja vya  Leaders Club, Kinondoni jijini Dar kwa ajili ya kuuaga mwili wa marehemu, hawakufanikiwa kufanya hivyo kwa sababu za kishirikina.
“Kwa kweli kilichotokea pale kwa watu wanaojua ushirikina unavyofanya kazi wataamini, yule mganga aliyemmaliza Kanumba alifanya kila njia, watu wakawa wanakanyagana, utaratibu ukafa, kwani angeruhusu watu wote kuaga kuna wengine wenye macho ya kiroho, wengine kichawi wangegundua Kanumba wa kwenye jeneza si binadamu,” alisema mwanafamilia huyo (jina linahifadhiwa).

AZIKWA NA BIBLIA
Hili nalo ni jipya, kwani kwa mujibu wa Mama Kanumba, baada ya kuambiwa mwanaye alichukuliwa msukule, familia iliamua kumzika sanjari na Biblia pembeni ili mwili wake usiondolewe kaburini na hao waliomchukua msukule.

BABA KANUMBA NA SIMU YA MWANDISHI
Alipotafutwa Baba Kanumba ili azungumzie tuhuma zilizopo za kutoa vitisho, aliomba kupigiwa baadaye kisha akakata simu.

KIKAO KIZITO SHINYANGA
Habari tulizozipata wakati tunakwenda mtamboni zinadai kuwa Jumamosi, familia ya Mzee Kanumba iliyopo Shinyanga ilikaa kikao kizito cha kumteua msimamizi wa mirathi ya mali za marehemu Kanumba.
Ijumaa Wikienda linaendelea kufuatilia kwa karibu kikao hicho ili kumpata mteuliwa na kumuanika.

0 comments:

Post a Comment