TIMU za soka Tanzania ‘Kilimanjaro Stars’ na Malawi ‘The Flames’
jana zimeshindwa kutambiana baada ya kulazimisha sare ya bila kufungana
katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo ulikuwa ni mahususi kwa timu hizo kujinoa kwa ajili ya
mechi zake za mchujo wa kuwania kucheza Kombe la Dunia Juni 2, ambapo
Stars itakuwa Ivory Coast, huku Malawi itakwaana na Kenya ambapo zote
zitacheza ugenini.
Katika mchezo wa jana timu timu hizo zilionekana kusomana zaidi ambapo
wachezaji wake walijaribu kufanya mashambulizi ya hapa na pale lakini
hayakuleta matunda yoyote.
Dakika ya 33 Joseph Kamwendo wa Malawi alikosa bao la wazi baada ya shuti lake kugonga mwamba.
Dakika ya 40 Kazimoto naye alishindwa kutikisa nyavu za Malawi baada ya shuti lake kupanguliwa na kipa, Simplex Nthala.
Mwamuzi wa kimataifa, Oden Mbaga, alimlima kadi ya njano Kamwendo katika dakika ya 43 baada ya kumchezea vibaya Kazimoto.
Malawi ilionekana kuishambulia zaidi Stars lakini jitihada za Kipa
Juma Kaseja ziliwezesha kuzuia nyavu zake kutikiswa. Hivyo kipindi cha
kwanza kumalizika kwa sare 0-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikionekana kuwa na
uchu wa kupata bao ambapo katika harakati hizo mshambuliaji wa Stars
Mbwana Samatta alikosa bao la wazi katika dakika ya 58 baada ya shuti
lake kutoka nje.
Mbaga alimzawadia kadi ya njano nyota wa The Flames, James Sangala, baada ya kumchezea vibaya Samatta.
Katika mchezo huo Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya bia Tanzania
(TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro ilimtoa Wazir Salum na kumuingiza
Amir Maftah, huku The Flames ikiwatoa Dave Banda, Zicco Mkanda, Russell
Mwafulirwa na kuwaingiza Jimmy Zakazaka, Amadu Ally na Ndaziona
Chatsalira.
Katika mchezo ambao hadi dakika 90 zinamalizika hakuna timu iliyoweza
kuliona lango la mwenzake, Kili Satrs inayonolewa na Mdenish Kim
Poulsen, ambaye jana ilikuwa ni kibarua chake cha kwanza tangu arithi
mikoba ya Mdenish mwenzake, Jan Poulsen, ilionekana na mabadiliko
makubwa na hasa wachezaji wake kuonekana wamepikwa vema.
Hata hivyo chipukizi waliomo katika kikosi cha Stars kama Frank Domayo
walionekana kutozoea mikiki, huku safu ya kiungo ikionekana
kutowasiliana vema na washambuliaji, wakati nafasi ya ulinzi nayo kidogo
ilionekana kuzubaa.
Stars: Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Wazir Salum/Amir Maftah, Aggrey
Morris, Kelvin Yondan, Shaban Nditi, Mrisho Ngasa, Frank Domayo, Mbwana
Samatta, Haruna Moshi ‘Boban’ na Mwinyi Kazimoto.
Malawi: Simplex Nthala, Limbikani Mzava, Moses Mvula, Foster Namwela,
James Sangala, Joseph Kamwendo, Frank Banda, Dave Banda/Jimmy Zakazaka,
Zicco Mkanda/Amadu Ally, Robin Ngalande na Russell Mwafulirwa/ Ndaziona
Chatsalira.
0 comments:
Post a Comment