Rais wa zamani nchini Liberia Charles Taylor amehukumiwa miaka 50 jela na makahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita.
Mwezi jana Taylor alipatikana na makosa ya
kuwaunga mkono waasi nchini Sierra Leone katika vita vya wenyewe kwa
wenyewe kati ya mwaka 1991 na 2002.
Upande wa mashtaka ulitaka kiongozi
huyo wa zamani kusukumwa jela miaka 80. Charles Taylor amesisitiza hana
hatia yeyote na anatarajiwa kukata rufaa.
Mwandishi wa BBC aliyeko The Hague Anna Holligan
anasema rufaa dhidi ya hukumu hii huenda ikachukua miezi sita. Akitoa
hukumu hiyo Jaji Richard Lussick amesema dhuluma zilizotekelezwa nchini
Siera Leone zilikuwa za kinyama zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia
ya binadamu.
Mahakama maalum ya Kimataifa inayochunguza
dhuluma za kivita nchini Sierra Leone ilimpata Taylor na hatia ya makosa
11 dhidi ya binadamu ikiwemo mauaji na ubakaji.
Taylor amekuwa Rais wa kwanza kuhukumiwa kwa
makosa ya vita na Mahakama ya Kimataifa tangu kesi za Nuremurgs dhidi ya
watawala wa Kinazi baada ya Vita Kuu ya Pili duniani.
Charles Taylor amelalamikia upande wa mashtaka
kwa kuwatisha mashahidi katika kesi dhidi yake. Rais huyo wa zamani
anatuhumiwa kwa kuwapa silaha waasi na kubadilishana na almasi.
Kesi dhidi ya kiongozi huyo wa zamani wa Liberia
inasikilizwa The Hague kwa hofu kwamba kufanyika kwake Sierra Leone
huenda kukazua vurugu katika kanda hiyo. Taylor anatarajiwa kuhudimia
kifungo chake nchini Uingereza.
CHANZO CHA HABARI: BBC SWAHILI
0 comments:
Post a Comment