Thursday, April 19, 2012


Waziri matatani

Sakata la upanuzi bandari
WAZIRI wa Uchukuzi, Omar Nundu
WAZIRI wa Uchukuzi, Omar Nundu
Wabunge wataka ang’oke, nyaraka zaanikwa
Atofautiana na Naibu na katibu Mkuu wake
Alitaka kuwazunguka Mkulo na Dk. Kawambwa
WAZIRI wa Uchukuzi, Omar Nundu, sasa anasubiri huruma ya Rais Jakaya Kikwete kuendelea na uwaziri baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kupendekeza avuliwe nafasi hiyo, imefahamika.
Kamati hiyo ya Bunge inamtuhumu Nundu kuhusika kukwamisha mradi mkubwa wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na kisha utetezi wake kushindwa kuishawishi kamati hiyo.
Hatua hiyo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu inakuja baada ya mwishoni mwa wiki kukutana hapa na wahusika wa sakata hilo akiwamo Nundu na uongozi mzima wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Bodi yake, kufikia uamuzi wa kutaka Nundu apishe.
Taarifa za suala hilo zinasema Kamati ilitaka maelezo kuhusiana na taarifa za kwamba Nundu amethubutu hata kukejeli maamuzi yaliyofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha, yakimhusisha Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo na watendaji wengine wa Wizara ya Uchukuzi.
“Nundu aliingia katika kikao na laptop yake bila ya kuwa na nyaraka zozote, wakati wabunge walikuwa na nyaraka na walipomhoji hakuwa na maelezo ya kuridhisha. Walimtaka aeleze ni kwa nini amefanya maamuzi kupingana na maamuzi yaliyokwisha kufanywa na Wizara yake na Wizara ya Fedha na pia walitaka kujua safari alizokwenda nje ya nchi zilikuwa na maslahi gani kwa nchi,” anasema Mbunge mmoja aliyehudhuria kikao hicho.
Katika kikao hicho, Mbunge mmoja ambaye amewahi kuwa waziri mwandamizi, alitoa mifano hai ya jinsi Serikali ilivyofanikisha miradi yake katika mtindo ambao Nundu anapingana nao, na akamuasa: “Mheshimiwa Waziri unapaswa kuangalia maslahi ya nchi kwanza.”
Awali katika kikao chao na Wabunge, Bodi na Menejimenti ya TPA ilitofautiana waziwazi na Waziri Nundu ikiorodhesha sababu nne za kumpinga Waziri Nundu pamoja na viambatanisho vinavyothibitisha sababu hizo.
Gazeti hili limefanikiwa kuona nakala za nyaraka mbalimbali, ikiwamo viambatanisho kadhaa, kuhusu mvutano huo ambao unaonyesha kuwa Waziri Nundu  ametofautiana hata na Naibu wake, Dk. Athumani Mfutakamba na Katibu Mkuu wake Omar Chambo.
Kiini cha mvutano huo inaelezwa kuwa baada ya kuteuliwa kuwa Waziri ni kama amekuwa akivuruga mipango ya kimaendeleo iliyowekwa na Waziri aliyemtangulia, Dk. Shukuru Kawambwa, kuhusu upanuzi wa Bandari.
Akiwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Kawambwa, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bandari, walitafuta mkopo kutoka Serikali ya China kupitia Benki ya Exim ya China iliyoridhia kutoa mkopo wa dola za Marekani takriban 524 ili zisaidie upanuzi wa gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam.
Kinachogomba katika mvutano huo ni uamuzi wa Waziri Nundu kumkataa mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo ambaye, Benki ya Exim imependekeza ndiye awe mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo. Mkandarasi aliyependekezwa na Benki ya Exim ya China ili itoe mabilioni hayo kama mkopo ni kampuni ya huko huko China inayoitwa China Communications Construction Company (CCCC).
Taarifa zinadai kwamba Waziri Nundu anadaiwa kuwa na mkandarasi wake ‘mfukoni’ ambaye ni kampuni nyingine ya China inayoitwa China Merchants, ambayo aliamua kuingia nayo Mkataba wa Makubaliano (MOU), bila kuwahusisha watendaji wake na TPA. Wasaidizi wake wote waligoma kushirikiana naye na akalazimika kumfukuza mmoja wa wakurugenzi wake, ambaye sasa amehamia Wizara ya Ujenzi.
“Waziri kwanza ameingia MOU na kampuni hiyo katika kipindi ambacho tayari Serikali imekwishakamilisha mchakato wa kupata fedha na kuanza kwa mradi. Cha kushangaza Waziri alipoulizwa alisema kampuni hiyo ilikuja Dar es Salaam na baadaye yeye kuwafuata China, lakini akashindwa kutoa maelezo ya kuhalalisha maamuzi yake,” anasema Mbunge mwingine wa kamati  hiyo.
Kutokana na ‘nguvu’ za kampuni hiyo inayopiganiwa dhidi ya CCCC, imeelezwa kuwa Serikali inaweza  kukosa mkopo huo unaotajwa kuwa wa riba nafuu ili kampuni mpya iendeshe si ujenzi wa mradi tu, lakini baada ya mradi iendelee kumiliki utoaji huduma bandarini kwa kushirikiana na wadau wengine kwa mkataba wa miaka 45.
Hali ilivyokuwa kabla ujio wa Nundu
Mipango inadaiwa kuwa safi wakati wa Waziri Shukuru Kawambwa, ni wakati huo ambao TPA iliandikia Wizara ya Uchukuzi (wakati huo Wizara ya Miundombinu) kuelezea mapendekezo ya kupanua Bandari.
Wizara iliafiki mapendekezo ya TPA na kuchukua hatua ambazo ni kuiandikia Wizara ya Fedha barua zenye zenye kumbukumbu namba CB 230/364/01/62 ya Aprili 14, 2010 na CCB 364/505/01/54 ya Julai 9, mwaka juzi (2010) ili ipate kibali cha kuomba mkopo kutoka Serikali ya watu wa China.
Wizara ya Fedha iliunga mkono kuendeleza mchakato huo kwa kuomba mkopo Benki ya Exim ya China, kupitia barua yenye kumbukumbu namba TYC/450/2/02 ya Februari 22, mwaka jana na nyingine yenye kumbukumbu namba TYC/E/450/2/130 ya Novemba 9, mwaka jana pamoja na barua ya Januari 24, mwaka huu, yenye kumbukumbu namba TYC/E/450/2/02.
Baada ya hapo, Wizara ya Fedha ilitaarifu Wizara ya Uchukuzi kupitia barua yake yenye kumbukumbu namba TYC/E450/2/02 ya Agosti 22, 2011 kuhusu kuridhia kupatikana kwa mkopo na kushauri kuwa TPA iendelee na mchakato wa kupata mkopo husika.
Kutokana na ‘kibali’ hicho kutoka Wizara ya Fedha, Wizara ya Uchukuzi ilitaarifu TPA kuendelea na mchakato wake wa kuomba mkopo kutoka Benki ya Exim.
Sababu za kuomba mkopo
Sababu za kuomba mkopo kwa ajili ya upanuzi huo wa gati za Bandari ya Dar es Salaam ni kwanza, mkopo utatolewa kwa Serikali ya Tanzania kwa masharti nafuu, ukiwa ni mkopo wa miaka 15 kwa riba ya asilimia mbili na kipindi cha mpito (grace period) ya miaka mitatu.
Mkopo huo unatajwa kuwa nafuu kutokana na ukweli kwamba, mikopo kutoka vyanzo vingine ina riba isiyopungua asilimia 5.5 na muda wake wa kurejesha ni mfupi ukiwa kati ya miaka mitano hadi 10.
Sababu ya pili  ni kwamba, mkopo kutoka Serikali ya China una masharti nafuu na mradi utakuwa na faida kwa maelezo kwamba, gharama za ujenzi zimekadiriwa kurejeshwa katika kipindi cha miaka 12 baada ya mradi kukamilika na hivyo faida yote kubakia kwa Mamlaka ya Bandari.
Sababu ya tatu ya kung’ang’ania mkopo huo inatajwa kuwa ni Serikali, baada ya ujenzi wa mradi itaweza kukodisha shughuli za biashara na kupata faida zaidi kutokana na TPA kuwa na uwezo wa kupanda kodi ya pango na mrabaha.
Sababu hiyo ya tatu inapingana na matakwa ya Waziri Nundu ambaye anataka ujenzi uendeshwe na kampuni nyingine ambayo pia baada ya ujenzi kukamilika itaendesha biashara na kujifidia gharama za ujenzi kwa miaka zaidi ya 45.
“Kama mradi huu utatekelezwa na kampuni binafsi, mwekezaji atahitaji kutumia gati kwa zaidi ya miaka 40 kabla ya kurejesha mikononi mwa Serikali. Kwa mfano, kampuni ya China Merchants imependekeza kujenga, kumiliki, kuendesha gati namba 13 na 14 kwa miaka 45.
TPA yamuumbua Waziri mbele ya wabunge
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Menejimenti ya Bandari imewasilisha waraka kwa wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu ikieleza kutoridhishwa na Waziri Nundu kuhusu usimamizi wake katika mradi huo.
 Waraka huo unaeleza; “menejimenti imetathmini hoja za Waziri wa Uchukuzi na haikubaliani nazo zote kwa ujumla wake”
Wanabainisha sababu za kutokukubaliana kuwa ni pamoja na; “Kampuni ya CCCC ilikuja kama mwekezaji wala si kama washauri (tofauti na anavyoeleza Waziri) na ilifanya upembuzi yakinifu kwa gharama zake na mradi huu unatakiwa kutekelezwa chini ya utaratibu wa Engineering Procurement and Construction (EPC) ambapo mwekezaji anatakiwa kufanya upembuzi yakinifu, usanifu (design) na kujenga.
Wanaeleza pia kuwa sababu nyingine kuwa ni kampuni ‘zinazopiganiwa’ na Waziri Nundu kwamba zitatekeleza mradi kwa gharama nafuu hazijathibitisha gharama halisi za mradi kwa sababu hazijafanya upembuzi yakinifu na kwamba gharama wanazotaja kuwa ni nafuu ni makisio tu.
Wanaendelea kueleza kuwa, kinyume cha kauli ya Waziri Nundu kwamba Waziri wa Biashara wa China anaunga mkono uamuzi wake (Nundu), menejimenti haina ushahidi wa hilo na kwamba ushahidi uliopo kuhusu kampuni ya China Merchants Holdings anayoipigania Nundu waliwahi kutaka kujitoa katika mradi baada ya kubaini tayari Serikali ilianza mchakato na kampuni ya CCCC kwa kutumia fedha za Exim.
 “Pamoja na hayo, sheria ya manunuzi ya umma namba 21 ya mwaka 2004 inaelekeza chini ya kifungu cha 4 (1) cha sheria hiyo kukubaliana na masharti ya utekelezaji wa mkataba pale Serikali zinapokubaliana jinsi ya utekelezaji wa manunuzi ya mradi husika. Hivyo kukubaliana na masharti ya mkopo ulioombwa kutoka Exim hakukiuki sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2004,” unaeleza waraka huo.
Mdau mmoja wa sekta ya bandari, alisema Waziri Nundu anapaswa kumpeleka mwekezaji anayemtaka kujenga bandari ya Mbegani, badala ya kulazimisha kumuingiza katika eneo la mradi ambalo tayari Serikali imekwisha kamilisha mchakato wake.
Kwa miezi kadhaa sasa Raia Mwema limekuwa likiandika utata katika upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, suala ambalo Waziri Nundu amekuwa akilitolea ufafanuzi kwa jazba, hadi kufikia kutoa matangazo ya kutetea uamuzi wake huo na kukejeli taarifa zinazopingana naye.

CHANZO CHA HABARI HII KUTOKA RAIA MWEMA.

0 comments:

Post a Comment