0digg
Mussa Juma na Peter Saramba , ArushaMWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kata ya Usa-River, wilayani Arumeru mkoani Arusha, Msafiri Mbwambo (32) ameuawa kinyama kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana.
Mamia ya wakazi wa Jiji la Arusha na Wilaya ya Arumeru jana, walifurika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, kushuhudia mwili wa Mbwambo ambaye pia, alikuwa fundi ujenzi .
Mbwambo aliuawa na watu wasiojulikana baada ya kupigiwa simu kumwita majira ya saa mbili usiku, wakati akitazama taarifa ya habari eneo la Mji Mwema akiwa na watu wengine.
Katibu wa Chadema wa Wilaya ya Arumeru, Dotnan Ndonde, alisema mara baada ya marehemu kuondoka muda mfupi baadaye, mwili wake uliokotwa eneo la Shule ya Mukidoma, Kusini mwa mji wa Usa-River umbali wa takriban kilomita mbili kutoka alipokuwa.
“Tulimkuta akiwa anavuja damu ilionekana muda si mrefu alikuwa amechinjwa na watu wasiojulikana ambao walikuwa wametoweka,”alisema Ndonde
Mwili wa kada huyo ulichinjwa kuanzia kisogoni na taarifa za uchunguzi wa madaktari jana zilithibitisha kuwa kifo hicho kimetokana na kuchinjwa.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Thobias Andengenye amethibitisha kutokea tukio hilo na kueleza kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi kuwapata wahusika waliofanya unyama huo.
Baadhi ya watu mjini hapa wamekuwa wakihusisha mauaji hayo na vuguvugu za kisiasa hasa baada ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, ambapo Chadema kiliibuka mshindi.
Hata hivyo Kamanda Andengenye amekanusha tetesi hizo na kuwataka wananchi wasubiri uchunguzi wa polisi .
Chadema wahusisha mauaji na siasa
Mbunge wa Arumeru Mashariki kupitia Chadema, Joshua Nassari na Katibu wa chama hicho Jimbo la Meru, Ndonde, walisema tukio hilo lina harufu za kisiasa.
Ndonde alisema kwa mazingira ya tukio na hali ya kisiasa eneo la Meru, anashindwa kuyatenganisha mauaji hayo na siasa.
“Wengi wanamjua marehemu alikuwa nguzo ya chama katika mji wa Usa ambapo Chadema tulipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mbunge. Anapouawa kwa kuchinjwa ghafla wakati vuguvugu la siasa likiendelea, sisi tunaamini ni mambo ya siasa,”alisema Ndonde.
Mbunge Nassari ameeleza kusikitishwa kwake na tukio hilo la kinyama na kusema kuwa bado joto la kisiasa lipo juu wilayani humo na kulitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linawasaka na kuwatia mbaroni wale wote waliofanya unyama huo.
Kwa upande wakev aliyekuwa Mbunge Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema alisema ana wasi wasi kuwa mauaji hayo ni mfululizo wa vifo vinavyoendelea kutokea, vikihusisha viongozi wa Chadema kila baada ya chaguzi ndogo.
“Tumeshuhudia watu watatu, wote wakiwa wanachama wetu wakiuawa baada ya uchaguzi mdogo wa Igunga na wengine kupotea katika mazingira ya kutatanisha,” alisema Lema.
Lema aliongeza kuwa baada ya uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki yamekuwepo matukio ya watu kuuawa, likiwemo lile la wiki iliyopita ambapo watu wanne walikutwa wamenyongwa hadi kufa katika eneo la Tengeru.
“Sasa hata wiki haijapita, mwenyekiti wetu wa Usa-River anauawa kwa kuchinjwa kinyama. Tunaomba vyombo husika vifuatilie matukio haya,” alisema Lema.
Marehemu Mbwambo, ameacha mke na watoto watatu.
Matukio mengine ya mauaji
Tukio la mauaji ya kada huyu limekuja ndani ya siku kumi baada ya mauaji mengine ya kinyama kutokea wilayani humo.
Aprili 21 mwaka huu, watu wanne walikutwa wamekufa kwa kunyongwa na watu wasiojulikana pembezoni mwa Mto Nduruma, katika maeneo matatu tofauti wilayani Arumeru.
Miili ya watu hao ambao ni wanaume waliokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 20-40, ilionwa na wakazi wa eneo hilo asubuhi ikiwa imetupwa.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha Andengenye alisema polisi wanachunguza tuko hilo na uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa watu hao waliuawa usiku wa kuamkia siku hiyo.
Andengenye alisema miili ya watu wawili iliokotwa eneo la Daraja la Gomba Estate, mwingine uliokotwa njia panda ya kwenda Mbuguni katika eneo la Chuo cha Mifugo Tengeru na mwili mwingine uliokotwa jirani na eneo la Sekondari ya Tengeru.
“Uchunguzi wa awali unaonesha watu hawa waliuawa kwa kunyongwa kwa kuwa kuna dalili za kuvunjwa shingo,” alisema Andengenye.
chanzo cha habari hii ni tovuti ya mwananchi.
0 comments:
Post a Comment