Sunday, April 29, 2012




BONDIA Francis Cheka ‘SMG’ kutoka Morogoro, kwa mara ya tatu mfululizo usiku huu amempiga mpinzani wake Mada Maugo kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya saba katika pambano lililokuwa la raundi 12, kwenye ukumbi wa PTA, Saba Saba, Dar es Salaam.
Maugo baada ya kupigwa ngumi nyingi katika raundi tatu mfululizo, kiasi cha kutabiriwa kukaa chini wakati wowote, mwanzoni mwa raundi ya saba hakurejea ulingoni.
Msaidizi wake, Karama Nyilawila alitupa taulo ulingoni akisema bondia wake hataendelea na pambano.
Refa John Shipanuka kutoka Zambia aliyelimudu pambano hilo, alimuinua mkono Cheka kumtangaza mshindi kwa TKO raundi ya saba.
Baada ya hapo, Maugo aliinuka kwenye kona yake na kwenda kumkumbatia Cheka na kocha wake, akisema kwamba amesalimu amri baada ya kuishiwa pumzi.
“Pumzi imekata, siwezi kuendelea,”alisema Maugo ambaye leo alionekana muungwana ingawa hakuwa tayari kusema atahitaji pambano la nne au la.
Akiwa mwenye furaha, Cheka alisema kwamba anamshukuru Mungu amemuwezesha kuendeleza ubabe wake kwa mabondia wa Tanzania na sasa anageuzia makali yake kwa Japhet Kaseba ambaye naye ameomba pambano la marudiano.
Katika pambano la leo, refa Shipanuka alimdhibitu Maugo mwenye desturi ya kuwakumbatia wapinzani wake ili kukwepa kupigwa na pia kupumzikia kwenye miili yao.
Kila alipokuwa akimkumbatia Cheka, Shipanuka alikuwa akifika na kuwaachanisha na kufanya mabondia hao watumie muda mwingi kupigana.
Pamoja na hayo, Maugo alilianza pambano hilo vizuri na katika raundi ya pili almanusra ashinde kwa Knockout (KO) baada ya kumkalisha mpinzani wake kwa ngumi kali.
Lakini SMG aliinuka na kuendelea na pambano, ingawa limchukua hadi raundi ya nne kuanza kuutawala mchezo.
Raundi ya kwanza hadi ya tatu, Maugo alifanya vizuri, lakini baada ya hapo mambo yalikuwa magumu na tangu hapo wengi walijua angepigwa wakati wowote.
Katika  mapambano ya utangulizi, mdogo wake Cheka, Cosmass Cheka alipigwa kwa pointi na Sadiki Momba katika pambano la uzito wa Light, wakati Hajji Juma alimpiga kwa pointi Emmilio Naffat uzito wa bantam.
Simba Watunduru alimpiga kwa KO raundi ya sita Mohamed Kashinde katika pambano la uzito wa Feather, wakati Amos Mwamakala alimpiga kwa pointi Said Muhiddin uzito wa Light.
Moro Best alimpiga Nassib Ramadhan kwa TKO raundi ya nne uzito wa Bantam na Salima Kabombora alimpiga Asha Ngedere kwa pointi uzito wa Bantam.
SOURCE-SHAFII DAUDA

0 comments:

Post a Comment