SAKATA la madai ya madereva wanaowaendesha wabunge wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania limezidi kuchukua sura mpya sasa wadai watayaanika majina ya wabunge waliofukuza madereva wao na kuifanya kazi hiyo wenyewe pamoja na wale ambao wanawalipa madereva wao chini ya shilingi 50,000 na wanaolipa vizuri madereva wao.
Kwani wamedai kuwa njia hiyo itawasaidia zaidi kujua umma kujua jinsi ambavyo wabunge hao wanavyoongoza kuwatetea wanyonge wakati wao wakiendelea kuwatendea ndivyo sivyo madereva wao.
Madereva
hao wamesema kuwa wabunge wamekuwa mbele kutetea madereva
wanaofanya kazi hiyo hapa nchini kupewa mikataba wakati kwa upande
wao wabunge hao wamekuwa wakiendelea kuwafanyia ufisadi kwa
kutowalipa fedha zao wala kuingia mikataba ya kisheria.
Uamuzi huo wa madereva hao kutaka kuwaanika katika vyombo
vya habari wabunge hao umetolewa leo tena ikiwa ni siku mmoja baada ya
mtamdao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com na gazeti la Jamboleo
kuandika juu ya madai ya madereva hao kwa mabosi wao ambao ni wabunge.
Mwenyekiti wa chama cha madereva wa wabunge wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania Juvenille Joseph alisema kuwa wapo baadhi ya wabunge wachache wa CCM na wale wa vyama vya upinani ambao wamekuwa wakiongoza kwa kuwajali madereva wao .
Ila alisema wapo baadhi ya wabunge ambao madereva wao hata kulala kwao na kula kwao wakiwa bungeni Dodoma ni shida na kuwa baadhi ya madereva wanaolipwa vizuri wamekuwa wakiwachangia fedha za kununua mihogo na maji .
Hivyo alisema kuwa uwazi wa madereva hao kwa kuanika majina ya wabunge wao ambao wamekuwa wakiwapunja haki zao itasaidia kupata haki yao badala ya kuendelea kuwa madereva wa majina na heshima wakati mfukoni hawana kitu.
“mbali ya wabunge kufanya kazi nao bila mikataba ila baadhi ya wabunge wamekuwa wakilipa vizuri akiwemo bosi wangu Felista Bulla (CCM) mimi kiukweli analipa vizuri sana tofauti na wenzangu ila bado nitaendelea kupigania haki ya madereva wenzangu …. Mimi wakati bunge la mwaka 2005 alinipa milioni 3”
Wabunge wengine waliotoa mkono wa ahsante kwa madereva
wao ni pamoja na mbunge Stella Manyanya ( CCM) Milioni 5.5 Zitto Kabwe
(Chadema) milioni 5.5 na mbunge mmoja wa viti maalum kutoka Zanzibar
yeye alimpa dereva wake milioni 3 japo hakurudi bungeni.
“Wabunge
wetu wanaongoza kwa kuikosesha serikali mapato yake na ajira kwa
vijana kupungua kutokana na baadhi yao kushindwa kutoa mikataba ya
kazi wala kuwalipa mishahara ambayo serikali kupitia bunge
ilipendekeza kwa ajili ya madereva wa wabunge toka mwaka 2008 .
Hata hivyo alimpongeza mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe (CCM) kuwa ameonekana kuwa mbunge aliyeingia bungeni kwa kipindi hiki cha kwanza na kuwa mfano wa kumjali dereva wake.
Madereva hao walisema
kuwa sehemu kubwa ya wabunge hao wameanza kuendesha magari yao
wao wenyewe baada ya kushindana na madereva waliokuwa wakiwaendesha
awali baada ya kushindwa kuwalipa mishahara na posho zilizobainishwa
kisheria na ofisi ya bunge.
Hata
hivyo walisema kuwa suala hilo la wabunge kushindwa kuwalipa
vizuri madereva si kwa wabunge wa CCM pekee bali ni wabunge karibu
wote wakiwemo wa vyama vya upinzani ambao baadhi yao kwa sasa
wanajiendesha wenyewe baada ya kukimbiwa na madereva wao kwa
kushindwa kuwalipa.
Pia
walisema matukio ya ajali kwa wabunge yamezidi kuongezeka kutokana
na wabunge hao kushindwa kufanya kazi na madeva na kuishia
kuifanya kazi hiyo wao wenyewe na matokeo yake kutokana na mawazo
ama kuwa na mambo mengi kichwani wamekuwa wakishindwa kuyamundu
magari yao na kuishia kusababisha ajali za barabarani ambazo baadhi ya
ajali hizo zimekuwa zikisababisha vifo ama ulemavu kwa wabunge hao.
“Leo
ukitazama hapa bungeni Dodoma utaona idadi kubwa ya wabunge
wanajiendesha wenyewe kama si mbunge kuwaendesha wenzake basi mbunge
amekuwa akijiendesha mwenyewe na wapo wanaokuja na madereva hadi hapa
Dodoma na baada ya hapo dereva amekuwa akipewa nauli ya kurudi
jimboni na mbunge anaendelea kujiendesha mwenyewe kama njia ya kubana
matumizi “
Aidha
walisema kuwa miongoni mwa madereva waliokosa ajira ni pamoja na
wale waliokuwa madereva wa mawaziri na manaibu mawaziri ambao
hawakurejea tena baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza mabadiliko ya
baraza la mawaziri hivi karibuni ambapo mawaziri hao kwa sasa
wamegeuka kuwa madereva wenyewe.
Makamu
mwenyekiti wa chama cha madereva wa wabunge wa bunge la jamhuri ya
muungano wa Tanzania Adam Said alisema kuwa sababu ya wabunge wengi
kukimbiwa na madereva ni kutokana na maslahi duni wanayoendelea
kulipwa na kuwa hivi sasa baadhi ya wabunge baada ya kukimbiwa na
madereva wamelazimika kuwatumia ndugu zao kama njia ya kukwepa
kuwalipa mishahara .
Pia
alisema maisha ambayo madereva hao wamekuwa wakiishi mjini Dodoma
ni heri ya omba omba kutokana na wabunge hao kuwalipa kiasi cha
shilingi 50,000 ama chini ya hapo na kutaka kuitumia kwa muda wa
wiki moja ama mwezi mzima jambo lililopelekea madereva hao kupanga
vyumba mtaani na kuishi katika chumba kimoja zaidi ya watatu kama
sehemu ya kubana matumizi.
Mwenyekiti
wa chama cha madereva wa wabunge wa bunge la jamhuri ya muungano
wa Tanzania Juvenille Joseph alithibitisha madaia ya madereva hao na
kuwa tayari uongozi wake umefikisha malalamiko ya madereva hao
katika ofisi ya chama cha wafanyakazi mkoa wa Dodoma pamoja na ofisi
ya spika wa bunge Anne Makinda ili kushughulikia madai hayo.
Alisema
kuwa kwa sasa wanakusudia kuitisha mkutano wa dharura wa madereva
wote wanaowaendesha wabunge ili kuweza kuwa na msimamo wa pamoja
katika kupigania haki zao na baada ya hao watawatumia barua wabunge
ambao wanajiendesha wenyewe ili waweze kujiunga na chama hicho cha
madereva wa wabunge .
Kwani
alisema kuwa katika barua iliyotolewa na ofisi ya bunge Novemba 3
mwaka 2008 barua yenye kumbukumbu namba FA.155/206/01/70 ikiwa na
kichwa yahusu posho ya ubunge Malimbikizo July –Octoba 2008
ilibainisha posho na mishahara hiyo.
Joseph
alisema kuwa posho ya mafuta lita 1000 kwa lita shilingi 2500 kwa
wakati huo ilikuwa ni kiasi cha shilingi milioni 2.5 kwa mwezi ,
Matengenezo yagari asilimia 40 ya thamani ya mafuta ambayo ilikuwa ni
milioni 1 kwa mwezi , posho ya dereva siku 10 kwa shilingi
30,000(vijijini ) ilikuwa ni shilingi 300,000 na posho ya mbunge siku
10 kwa kila atakazokuwepo kijijini kwa kila siku shilingi 45,000
ilikuwa ni shilingi 450,000 huku mshahara wa dereva kwa mwezi
ulikuwa ni shilingi 100,000 na kufanya jumla kwa mwezi kuwa bajeti
ya shilingi milioni 5,115,000 kwa wakati huo.
Ila
pamoja na sasa posho za wabunge kupanga ila bado wabunge
wamekuwa wakiwalipa madereva wao kiasi cha shilingi 70,000 hadi 90,000
kwa mwezi fedha ambazo haitoshi kwa maisha ya sasa hivyo kutaka
fedha za madereva kuingizwa katika akaunti zao na madereva wote wa
wabunge kuwa na mikataba ya kazi badala ya kuendelea kufanya kazi
kirafiki na kindugu.
Wakati huo huo mbunge wa jimbo la Ludewa Filikunjombe amewataka amefunguka kulizungumzia suala hilo na kuwataka madereva hao kuacha uoga na iwapo hawalipwi kweli kuwa wawazi na kuepuka uoga wa kuwataja kwa majina wabunge wao.
Hata hivyo uchunguzi wa mtandao huu wa www.mangiayoub.blogspot.com umebaini sehemu kubwa ya wabunge wa vyama vya upinzani na waliokuwa mawaziri na manaibu waziri katika baraza la mawaziri lililobadilishwa hivi karibuni ndio wanaongoza kwa kujiendesha wao wenyewe baada ya kushindwa kuwalipa mishahara madereva wao.
USIKOSE GAZETI LAKO LA JAMBOLEO KESHO JUMAPILI KWA UNDANI WA HABARI HII
0 comments:
Post a Comment